
MCHUNGAJI wa kanisa la Neno Evangelism, James Maina Ng’ang’a ameendeleza mashambulizi yake dhidi ya baadhi ya Wakenya ambao wamekuwa wakimshambulia mitandaoni.
Ng’ang’a amekuwa akishambuliwa mitandaoni kwa takribani wiki 3 sasa baada ya video kuibuka mitandaoni ikimuonyesha jinsi alimfukuza kwa dharau mwanamke mmoja kutoka kanisa lake.
Katika video hiyo, mwanamke huyo kwa jina Milka Moraa Tegisi alikuwa ameenda kutafuta msaada wa kodi ya nyumba yake ambayo ilikuwa imefungwa.
Ng’ang’a alimlipua kwa ukali akimwambia kwamba hapo si pa kutafuta msaada ya hata kumuelekeza kuenda kutafuta msaada kwa nyumba za bei nafuu zinazojengwa na serikali kupitia mpango wa Boma Yangu.
Baada ya video hiyo kuibua huruma mitandaoni, afisa mmoja wa polisi – Sammy Ondimu Ngare, alijitoa kimasomaso kuwaongoza Wahisani wema kumchangia Moraa hela kwa ajili ya kutatua matatizo yake ya kodi ya nyumba.
Kando na kuongoza michango, Ondimu alimsaidia Milka kupata kazi katika mgahawa mmoja lakini pia kumkutanisha na waziri wa ardhi Alice Wahome aliyeahidi kumkabidhi mama huyo nyumba yake kupitia Boma Yangu katika kipindi cha wiki 2.
Hata hivyo, harakati za afisa huyo wa polisi kumsaidia Milka zilionekana kumkera mchungaji Ng’ang’a ambaye katika mahubiri yake wikendi iliyopita, aligeuza mtutu wake wa mashambulizi kwa polisi huyo.
Katika klipu ambayo afisa huyo wa polisi alichapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook, Pasta Ng’ang’a anaonekana akimfokea vikali akimwambia kwamba yeye hana hata pikipiki wakati yeye [Ng’ang’a] anateleza kwa gari la kifahari aina ya Lexus.
“Kama ni mtu mwingine mimi huwa siongei, lakini afisa wa polisi…sasa Ondimu hata ukatokezea hapa, hata ndevu huna. Hata huna pikipiki wewe, mimi niko na Lexus 600.”
“Tafuta rika lako mcheze nao, wale wahubiri ambao mmetahiri nao,” Ng’ang’a alihubiri huku akitoa onyo kali kwa polisi huyo dhidi ya kutojaribu tena wakati mwingine.
Awali, Ng’ang’a alikashifu vikali baadhi ya watu waliokuwa wakimtupia cheche kwa kitendo alichomfanyia Milka kumfukuza kanisani.
Kwa mujibu wa mchungaji huyo, alihoji mbona watu hawazungumzii idadi kubwa ya watu ambao amesaidia katika kanisa lake lakini hiki kisa kimoja tu ndicho kila mmoja anamhukumu nacho.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!