Kennedy Rapudo, Amber Ray na wanao kwenye picha ya pamoja

MJASIRIAMALI Kennedy Rapudo amepuuzilia mbali tetesi za watu wa mitandaoni kwamba yeye anafadhiliwa kimaisha na mkewe Amber Ray.

Alisema kwamba yeye si mtu asiye na pesa kwani mkewe mwenyewe ni shahidi ambaye muda wote amekuwa akiweka wazi kwamba hawezi chumbiana na mtu asiye na fedha.

“Mimi nalipa bili katika ile nyumba kwa sababu ni wajibu wangu. Amber Ray amejieleza kila mara kwamba hawezi chumbiana na mwanamume hana pesa. Hivyo kwa nini mimi niwe mwanamume wa kwanza kuwekwa na yeye?” alisema huku akikanusha madai ya kufadhiliwa kimaisha na Ray.

Mfanyibiashara huyo ambaye ni msiri katika biashara zake na vyanzo vya mali yake alifichua kwamba huwa hajishughulishi na kuwajibu au kuwachukulia watu wa mitandaoni hatua kwa kutoa kauli za uongo dhidi yake.

Kwa mujibu wa Rapudo, wengi mitandaoni wanasema tu kauli zisizo na mashiki na ambazo zikiradidiwa kwa muda wengi hufikiria ni za kweli.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Alisema kwamba hata ameona juzi mmoja akitoa kauli ya uongo bila kujua hata kiasi cha bili zinazotumika katika nyumba yake.

Kwa muktadha huo, Rapudo alifichua kwamba nyumba yake ina mahitaji ya bili za maelfu ya pesa ambazo wengi hawajui, akitolea mfano kwamba wanao 4 wanagharamiwa karo ya muhula karibia milioni.

Rapudo alifichua kwamba wanawe 4, akiwemo mdogo kabisa (Africana) wote wanasoma katika shule za Mtaala wa Uingereza na karo jumla kwa muhula mmoja inakaribia shilingi milioni.

“Huwa sijibu uchafu, niliona mmoja juzi akisema kwamba huwa natoa sijui laki moja… hiyo hata haikaribii bili za nyumba ile. Tuna watoto 4, ukihesabu mpaka Africana, na wote wanasomea katika shule za mtaala wa Uingereza. Unajua inagharimu pesa ngapi kwa muhula? Takribani milioni moja!”

“Uliza mtu yeyote mwanawe anasomea shule za aina hiyo, ni shule ghali sana. Hivyo ni nini ambacho 300k zitafanya kwetu au kubadilisha? Hakuna,” alisema huku akikanusha vikali kuhusika katika biashara ya utakatishaji hela.

Mfanyibiashara huyo alieleza kwamba nyumba yake mahitaji ya ndani pekee ni ghali na ni jukumu lake kuyafanya na hilo halimaanishi kwamba mkewe hana hela.

Alikanusha dhana inayoenezwa kwamba yeye na mkewe wamegawanya majukumu katika nyumba yake.

“Shopping pekee katika nyumba yangu kwa mwezi ni takribani Sh200k. Amber Ray hata hanunui chumvi. Si kwamba hawezi lakini ni kwa sababu ni wajibu wangu kama mume.”