Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi alishindwa kusoma ujumbe wa rambirambi wa Rais William Ruto wakati wa mazishi ya mwanawe aliyekuwa Seneta wa Embu Lenny Kivuti, Eric Kivuti siku ya Ijumaa.

 

Rais hakuweza kuhudhuria ibada hiyo kwa kuwa alikuwa katika mazishi ya mamake Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula huko Bungoma.

 

Hata hivyo, alikuwa ameandika ujumbe wa kusomwa kwa familia na waombolezaji.

 

Wakati Waziri Muturi aliposimama kusoma ujumbe huo, umati ulianza kupiga kelele, hivyo ikawa vigumu kwake kuendelea.

 

"Nimepewa ujumbe wa rambirambi, kutoka kwa Mheshimiwa Rais... (kelele) Sasa pale nimefika mwisho ni kwamba nimepewa ujumbe. Niwapatie. Nisome ama nisisome?" Muturi aliuliza

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

 

Umati ulijibu kwa kusema "Usisome".

 

Waziri alionekana akimshirikisha Askofu aliyekuwa akiongoza ibada kabla ya kuendelea.

 

"Nimeshauriwa kwa busara na unajua kama spika wa zamani… na mnajua marehemu JJ Kamotho, aliwahi kusema kuhusu kura ya makelele, nimeskia kura ya makelele.... Niko na heshima kufikisha ujumbe huu kwa Mhe lenny Kivuti hadharani,” alisema.

 

Muturi alikiri jibu lao, akieleza kuwa alikuwa ameshauriwa kusoma ujumbe huo hadharani.

 

Eric Mutugi Kivuti aliaga dunia wiki jana katika hospitali ya MP Shah baada ya kuugua kwa muda mfupi.

 

Hii si mara ya kwanza kwa waombolezaji kukataa kusomewa jumbe za rambirambi za Rais Ruto  wakati wa mazishi.

 

Mnamo Novemba 2024, wakati wa mazishi ya marehemu MCA Mark Gicheru Wainaina, kisa sawia kilitokea.

 

Wakati huo, Rais Ruto alikuwa ametuma Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata na Seneta wa Kirinyaga James Murango kusoma risala zake za rambirambi.

 

Hata hivyo, waombolezaji walianza kuzomea mara moja Murango alianza kutoa risala za rambirambi kutoka kwa Naibu Rais Kithure Kindiki kwa familia, marafiki na waumini wa kanisa waliohudhuria.