
Mwanamke aliyetoweka nyumbani kwa familia yake huko Gikono, Kabati, Kaunti ya Murang’a mnamo Desemba 23, amepatikana akiwa hai.
Lilian Nyambura Mbugua, 28, alipatikana katika kituo cha kujaza mafuta katika Mji wa Maragua, Murang’a mapema Jumanne, dakika kadhaa usiku wa manane.
Mjombake George Njuguna alisema alikuwa dhaifu na alionekana kuchanganyikiwa walipompata.
“Anasema alijipata kwenye kituo cha kujaza mafuta na kuwaambia wahudumu waliokuwa zamu wampigie simu mama yake. Tunawasiliana na mwajiri wake na anatazamiwa kupelekwa Nairobi kwa matibabu zaidi huku polisi wakiendelea kuchunguza kisa hicho,” Njuguna alisema.
Lilian alisafiri hadi nyumbani kwa mamake Jumamosi, Desemba 21, kwa ajili ya sherehe za Krismasi.
Mambo yalikuwa sawa na hata walihudhuria ibada ya kanisa pamoja Jumapili, Desemba 22, kabla ya kurudi nyumbani.
Alishiriki chakula cha mchana pamoja na familia siku iliyofuata, Jumatatu.
Kisha mnamo saa kumi na moja jioni, Lilian alitoka nje ya boma lao katika jumuia yenye milango kwa kile ambacho familia inasema kilionekana kama matembezi ya jioni.
"Ilionekana kana kwamba alikuwa ameenda tu kwa matembezi ya kawaida kuzunguka shamba hilo kwa sababu alikuwa bado amevaa kitambaa na slippers. Mamake alikuwa akifanya kazi za nyumbani nyuma ya nyumba,” Njuguna alisema.
Walipojaribu kumtafuta Lilian kwa kutumia simu zake mbili za mkononi, walikuta ameviacha vidude vyote viwili ndani ya nyumba kabla ya kuondoka.
"Gari lake, funguo zake, kompyuta ndogo na funguo za nyumba yake Nairobi pia vilikuwa katika nyumba ya familia, pamoja na hati zake zote za utambulisho," aliongeza mjombake.
Familia ilimngoja Lilian bila mafanikio na kuripoti kisa hicho kwa kituo cha polisi cha Gikono kilicho karibu Jumanne, Desemba 24 alasiri.
Pia waliripoti kwa Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) huko Kenol, ambayo Jumamosi, Desemba 28, ilifikia kusema uchunguzi umebaini hadi sasa Lilian alipiga simu tatu Jumamosi jioni, siku mbili kabla ya kutoweka.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!