
Rais William Ruto amesisitiza azma yake ya kuunganisha nchi kwa kuwaleta viongozi wote pamoja kwa ajili ya umoja na amani.
Ruto alisema viongozi wanapaswa kuungana ili kutoa mwongozo na uongozi kuhusu jinsi taifa linafaa kuendeshwa.
Alitamka haya baada ya kuhudhuria ibada ya kanisa huko Koiwa AIC kaunti ya Bomet siku ya Jumapili.
Rais alitoa wito kwa Wakenya kuweka kando siasa za ubaguzi na kujitahidi kuleta umoja kama taifa.
“Nimeamua na nimedhamiria kuunganisha Kenya. Watu wa Bomet, nawauliza, je, niendelee kuunganisha nchi, au tuwe nchi iliyogawanyika?” Rais Ruto aliambia mkutano wa hadhara kando ya barabara.
Alitoa wito kwa Wakenya kuunga mkono mipango ya maendeleo ya serikali yake katika maeneo ya barabara, kawi, afya na elimu.
"Ninawaomba muwe na umoja katika kuunga mkono miradi hii ili vijana wetu wapate ajira na nchi isonge mbele," Ruto alisema.
Rais pia aliwataka wakazi kumtumikia Mungu bila kuchoka. “Mbali na jitihada tunazoweka katika maisha yetu ya kila siku, pia kuna Mungu mbinguni ambaye ana mchango mkubwa katika mafanikio yetu.”
Katika ibada hiyo, Rais alitoa wito kwa waumini kuiombea nchi wakati wa kukaribisha mwaka 2025.
Aidha amewataka Wakenya kutafakari mafanikio ya utawala wake kufikia sasa na changamoto ambazo nchi imeshinda.
“Mwaka huu ulipoanza, mipango yetu mingi ilikuwa haijakamilika, lakini nina furaha kuwa hadi sasa, miradi kama vile ujenzi wa masoko inaendelea vizuri nchi nzima; mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu unaendelea vizuri na zaidi utawekwa mwaka ujao,” alisema Ruto.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!