
Babake mwanablogu wa Uthiru aliyetekwa nyara Peter Muteti ameomba radhi kwa yeyote ambaye alihisi kukasirishwa na mwenendo wa mwanawe kwenye mitandao ya kijamii.
Muteti alitekwa nyara na wanaume wasiojulikana ambao walificha nyuso zao mnamo Desemba 21 wakiwa katika duka moja huko Uthiru, Kaunti ya Nairobi .
Huku akitoa wito kwa serikali kusaidia kutatua kitendawili cha kutekwa nyara kwa mwanawe, Barnabas Njeru alisema kutekwa nyara kwa mwanawe kumemtia kiwewe yeye na familia yake kwa ujumla.
"Nilishtuka Desemba 21 nilipopokea taarifa kwamba mwanangu ametoweka. Tangu wakati huo nimekuwa na wasiwasi jamani," alisema.
“Ikiwa kijana huyo alikosea, basi naomba msamaha kwa niaba yake. Pia nataka kuwaomba Wakenya msamaha,” aliongeza baba huyo aliyefadhaika.
Huduma ya Kitaifa ya Polisi imekana kuhusika na madai ya utekaji nyara. Mamake Muteti Doricate Njeru alitilia maanani suala hilo akisema kutoweka kwa mtoto huyo kumezua wasiwasi katika familia.
Anasema hawajawahi kujua amani tangu hajulikani aliko. “Sijapata chakula kwa sababu sina amani, yamekuwa machozi tangu alipopotea, naomba serikali itusaidie ili mtoto wetu aachiliwe,” aliomba.
Siku ambayo Muteti alipotea, mwanablogu mwingine Billy Mwang alichkuliwa na watu wasiojulikana huko Embu.
Alikuwa kwenye kinyozi wakati watekaji nyara walipoingia, wakamtoa nje na kumfunga kwenye gari la kubebea watu wawili.
Wengine wanaosemekana kutoweka ni Bernard Kavuli, aliyetoweka Nairobi, Steve Mbisi aliyetekwa nyara Machakos, Gideon Kibet almaarufu Kibet Bull aliyetekwa nyara baada ya mkutano na seneta na Ronny Kiplang’at aliyetoweka Kiambu.
Utekaji nyara huo umezua taharuki kubwa kwenye mitandao ya kijamii huku Wakenya wakitaka waachiliwe.
Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya imesema jumla ya watu 82 wametekwa nyara tangu Juni mwaka huu huku 29 wakiwa bado hawajapatikana. Mnamo Desemba, watu saba waliripotiwa kutekwa nyara.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!