Henry Omondi, kijana aliyevuma sana kutokana na video ya ‘Ameuza aiport’ ni mvulana mwenye furaha baada ya kurekebishwa meno yake.

Habari njema kuhusu kutengenezwa kwa meno ya Henry ilitangazwa na mchekeshaji Eric Omondi ambaye amekuwa akimsaidia sana tangu akipomtafuta baada ya video yake akilalamika kuhusu Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kuuzwa kwa Mhindi kusambaa.

“HATIMAYE, TUMEPATA MENO MAPYA KWA NDUGU YETU??☺️????????? Asante sana kwa Daktari wa meno katika Hospitali ya Port Florence iliyoko Kisumu St Stephen’s Cathedral ACK????,” Eric alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Eric aliambatanisha taarifa hiyo na video ya Henry akiwekwa meno mengine na baadaye kuonyesha tabasamu lake jipya baada ya utaratibu huo.

Mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill pia alitangaza kuwa kijana huyo ambaye alivuma wakati wa maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali atafurahia kusafiri sehemu mbalimbali za dunia.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

"Tutaenda naye kwa Ndege Ulimwenguni kote ili tu kumwambia asante," alisema.

Mwezi uliopita, Henry alifunguka kuhusu maisha yake katika mahojiano ya kipekee na Radio Jambo.

Katika mahojiano hayo, kijana huyo ambaye alisema ana umri wa miaka 19, alijibu swali ambalo wengi walikuwa wakijiuliza tangu aanze ku-trend wakati wa maandamano ya nchi nzima; Jinsi gani alipoteza meno yake ya mbele?

Henry alisimulia jinsi meno yake yalivyovunjika akieleza kwamba alianguka chini baada ya kuruka na mdomo wake kugonga chini.

“Nilikaa Kisumu kabla nikuje Nairobi. Siku moja mtu aliniokota na kunipeleka katika kituo cha polisi cha Nyalenda. Vile nilifika huko, hao askari wakaninunulia chakula, maji, na wakaninunulia kila kitu. Alafu wakaniweka nyuma peke yangu. Nilikaa huko ndani walitaka kunipeleka rumande, nikahisi sitaki kurudi huko juu nimewahi kuwa huko tena. Nilihisi kuruka. Nilitarajia kuruka kwa matuta, sikuruka. Vile nilitaka kuruka nilitupa maji yangu na nini, kufika mbele kitu ikinifunika macho nikashtukia nisharuka.  Nikaruka kwa uvimbe, nikaruka na mdomo wangu,” Henry alisimulia.

Kijana huyo alisema mpita njia alimchukua na kumpeleka nyumbani kwake kwa ajili ya huduma ya kwanza kabla ya kumpa chakula ambacho alikataa.

Alisema kisha alipelekwa kwenye nyumba ya watoto ambako alikaa kwa muda.

Henry alijipatia umaarufu wakati wa maandamano ya Gen-z katikati ya mwaka huu kwa kupinga vikali uuzaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Sauti yake kubwa na shauku yake wakati wa majaribio ya kuandamana hadi JKIA katika lengo la kupinga kuuzwa kwake vilimfanya kuonekana sana na video yake imekuwa ikivuma kwenye mitandao ya kijamii tangu wakati huo.

Akizungumzia maisha yake, alifichua kuwa anatoka eneo la Nyanza.