Klabu ya West Ham inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza imezama katika maombolezo.
Klabu hiyo yenye maskani yake jijini London inaomboleza kufuatia kifo cha mlinda mlango chipukizi Oscar Fairs ambaye aliichezea timu yao ya wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 15.
Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 15 alipoteza maisha siku ya Ijumaa, Desemba 13, baada ya kupigana kishujaa na saratani. Alikuwa amepatikana na uvimbe wa ubongo mnamo Agosti 2023.
"Ni kwa masikitiko makubwa kwamba West Ham United inathibitisha kifo cha mlinda mlango wetu wa Akademi ya U15 Oscar Fairs, kufuatia vita vyake vya kijasiri na saratani. Pumzika kwa amani, Oscar jasiri,” West Ham ilitangaza kupitia mtandao wa kijamii Ijumaa jioni.
Klabu hiyo ilimtambua marehemu Oscar kama Hammer wa kikweli na kijana mzuri ambaye alipendwa na kila mtu katika Akademi yao.
Kama ishara ya heshima kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 15, mechi zote zilizopangwa za akademi wikendi hii zimeahirishwa.
"Kwa wakati ufaao, Klabu pia itashiriki habari kuhusu mipango yetu ya kumuenzi Oscar, na tutahakikisha kwamba jina lake halisahauliki kamwe akiwa West Ham United," taarifa hiyo ilisema.
"Mawazo na rambirambi za dhati za kila mtu kwenye Klabu ziko kwa wazazi wa Oscar, Natalie na Russell, na kaka yake Harry, na tunaomba kwa fadhili ufaragha wa familia uheshimiwe katika wakati huu mgumu sana," ilisoma zaidi.
Siku ya Ijumaa, timu ya kwanza ya West Ham ilinyamaza kwa dakika moja wakati wa mazoezi ya Ijumaa kwa ajili ya kumuenzi ya marehemu Oscar Fairs.
Habari za kifo cha Oscar zinakuja takriban wiki moja baada ya klabu hiyo yenye maskani yake London kutangaza kwamba mshambuliaji wake Michail Antonio alikuwa amehusika katika ajali ya barabarani.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Jamaica bado anaendelea na matibabu hospitalini baada ya ajali hiyo iliyotokea Jumamosi iliyopita.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!