Naibu rais aliyetimuliwa Rigathi Gachagua anadai kuwa tayari alikuwa amemuonya Rais William Ruto dhidi ya kukaribisha kampuni ya Adani Group nchini Kenya.

 Akizungumza Jumapili, Gachagua alisema tayari alikuwa ameona maovu katika mikataba ya Adani na akamfahamisha rais kuyahusu.

 Gachagua alifananisha mikataba hiyo yenye utata na kuipiga mnada nchi na akabainisha kuwa Wakenya waliipinga.

 “Mimi nilimwambia rais Ruto maneno ya Adani, ilikuwa ya kutiliwa shaka, iko na ukora. Huu ni kupiga nchi mnada, na watu hawataki," Gachagua alisema.

Gachagua alizungumza katika kanisa ya AIPCA Kangari katika eneo  laKigumo, kaunti ya Murang'a, ambapo alihudhuria ibada ya Jumapili akiwa na washirika wake wa karibu.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

 Alisema kuzungumza dhidi ya mikataba ya Adani na miradi mingine yenye shaka ndiyo ilivunja uhusiano wake na rais Ruto.

 “Ilisemekana ati mimi napinga miradi ya serikali. Sasa, ufisadi ni mradi wa serikali? Huo ni ufisadi, sio mpango wa serikali. Mimi nilipelekwa pale senate, mliskia mashtaka? Ati mimi nimekosea kuinua heshima kwa sababu mambo mengine napinga. Mambo haya ya Adani nilisema ni mbaya,” alisema.

 Gachagua alisema rais hastahili kupongezwa kwa kufutilia mbali mikataba hiyo, akibainisha kuwa hatua hiyo haikutoka moyoni mwake.

 "Alichukua hatua tu baada ya mshukiwa huyo kufunguliwa mashtaka nchini Marekani. Haikutoka moyoni mwake,” alisema.

 Naibu rais huyo wa zamani alimtaka rais kuwasikiliza watu wa Kenya kila mara na kukumbatia ukweli kila wakati.

Akizungumzia uhusiano wake na Ruto alipokuwa naibu wake, Gachagua alibainisha kuwa ni yeye pekee aliyekuwa na ujasiri wa kumrekebisha mkuu wa nchi au kumshauri kuhusiana na masuala mbalimbali.

“Hii maneno ya Adani na mengine ilifanya mimi na rais tukawa hatuelewani. Pale katika baraza la mawaziri, ilikuwa ni mimi tu naweza kumwambia rais ukweli. Wengine wote ni waoga. Akikondoa macho hivi, wote wanaenda chini,” alisema.

Gachagua alidai kuwa hata Mawaziri walikuwa wakimwendea na kumtaka amwambie rais kila walipohisi kuna jambo si sawa.

Naibu rais huyo wa zamani sasa amelitaka kanisa kuendelea kuikosoa serikali kila pale mambo yanapokuwa si sawa, huku akibainisha kuwa viongozi serikalini hawako tayari kuzungumza dhidi ya rais.