Naibu rais aliyetimuliwa Geoffrey Rigathi Gachagua ameibua madai ya dhuluma na vitisho kutoka kwa serikali ya Kenya Kwanza, takriban mwezi mmoja baada ya kutimuliwa afisini.

Katika taarifa yake Jumatano, mbunge huyo wa zamani wa Mathira alidai kuwa baadhi ya maajenti wa usalama wamekuwa wakimfuata kila mahali huku wakiendesha magari yasiyosajiliwa.

"Wanaegesha kwenye lango la makazi yangu ya Nairobi, wakifuatilia wageni wangu wote, na wananifuata kila ninapotoka nyumbani, hata hadi nyumbani kwangu huko Nyeri," Gachagua alisema kupitia mtandao wa kijamii.

Mwanasiasa huyo alidai kuwa gari ndogo, ambalo alionyesha maelezo yake, lilimfuata hadi kanisa la PCEA Kerarapon siku ya Jumapili. Gari hilo linadaiwa kumfuata hadi alikoenda kula chakula cha mchana na hata alipokuwa akirudi nyumbani.

"Baada ya kuangalia tovuti ya NTSA, niligundua kuwa nambari hizo zimesajiliwa kwa lori," alisema.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Gachagua alilalamika kwamba uchunguzi na vitisho kama hivyo kwa raia vilishuhudiwa mara ya mwisho katika enzi ya Moi miaka mingi iliyopita.

Kwa mara nyingine, aliwataka Wakenya kuiwajibisha serikali iwapo lolote litamtokea.

“Katika enzi hizi za mauaji ya kiholela, utekaji nyara wa kulazimishwa na kutoweka na maafisa wa serikali, nimeona ni muhimu kushiriki na Wakenya unyanyasaji na vitisho ninaopitia, na kuwafahamisha kuwajibisha serikali ikiwa nitadhuriwa na maafisa wa serikali, ” alisema.

Naibu rais huyo wa zamani aidha ameiomba serikali kumpa amani na kumruhusu kufurahia haki zake kama raia wa kawaida.

“Naomba serikali iniache! Mlinifukuza afisini, na sasa mnapaswa kuniruhusu kufurahia amani yangu kama raia wa kibinafsi,” Gachagua alisema.

Mnamo Oktoba 18, Gachagua alikuwa naibu wa kwanza wa rais kuondolewa mamlakani kwa njia ya kutimuliwa tangu kuzinduliwa kwa katiba ya Kenya ya 2010.