Siku ya Jumatano, Bilionea wa India Gautam Adani na watendaji wengine kadhaa walishtakiwa katika jiji la New York, Marekani kwa madai ya kuhusika katika mpango wa ulaghai wa mabilioni ya dola.

Kulingana na shirika la habari la CNN, Idara ya Sheria ya Marekani mnamo Jumatano ilisema kwamba Adani na wasimamizi wengine saba wakuu wa biashara waliahidi zaidi ya dola milioni 250 (Sh32.4b)  za hongo kwa maafisa wa serikali Wahindi ili kupata kandarasi za nishati ya jua.

Watendaji wengine walioshtakiwa pamoja na Adani ni pamoja na mpwa wake Sagar Adani.

Naibu Mwanasheria Mkuu Msaidizi Lisa Miller alisema kuwa hongo hizo zilikusudiwa kuwadanganya wawekezaji na benki ili kupata mabilioni ya dola, na kuzuia haki.

Mashtaka ya jinai, yaliyowasilishwa Jumatano mjini New York, ni pigo la hivi punde kwa Bw Adani mwenye umri wa miaka 62, mmoja wa watu tajiri zaidi nchini India, ambaye biashara yake inaenea kutoka bandari na viwanja vya ndege hadi nishati mbadala.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Ripoti za uchunguzi huu wa hongo zimekuwa zikizunguka kwa muda sasa.

Waendesha mashtaka walisema Marekani ilianza kuchunguza kampuni ya Adani Group mnamo 2022, na ikapata uchunguzi huo umezuiliwa.

Kundi la Adani, ambalo linaongozwa na Guatam Adani kwa muda limehusishwa na mikataba ya nishati na uwanja wa ndege nchini Kenya.

Mnamo Oktoba 11, 2024, Katibu wa Baraza la Mawaziri la Nishati na Petroli Opiyo Wandayi alitangaza kutiwa saini kwa mkataba wa mabilioni ya shilingi kati ya KETRACO na Adani Energy Solutions Limited.

Wandayi alisema kuwa makubaliano hayo, ambayo yanakadiriwa kuwa Sh95.68 bilioni (USD 736 milioni), yatashuhudia kampuni ya India ikiendeleza, kufadhili, kujenga, na kuendesha njia muhimu za kusambaza umeme na vituo vidogo kote nchini.

Alibainisha kuwa makubaliano hayo yanalenga kukabiliana na kukatika kwa umeme kwa muda mrefu nchini Kenya na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika ili kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi na matarajio ya viwanda.

Alibainisha kuwa, katika kipindi cha miaka 30 ijayo, Adani atasimamia miundombinu chini ya mkataba huo, na kuhakikisha uendelevu wake wa muda mrefu kabla ya kuuhamishia KETRACO.