SENETA maalum Karen Nyamu amezua utani kwenye mitandao ya kijamii jinsi inbox zake zimefurika baada ya kudaiwa kwamba ana deni la mwenye nyumba yake.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Nyamu alichapisha picha yake akidai kwamba kuna watu wanaojidai kuwa waganga ambao wamejaza inbx yake kwa jumbe za kutaka kumpa msaada.

Seneta huyo wa UDA alisema kwamba wengi wao wanajidai kuwa waganga wakimtaka kutuma shilingi elfu 20 na picha ya mlango wa nyumba yake ili waipigie ramli ya kumfanya mwenye nyumba kusahau kama anamdai.

“Ati nauza dawa ya kufanya landlord asahau rent, tuma tu 20k na picha ya mlango wako??️??️ Hawa waganga kutaka kulipua inbox yangu jameni,” Karen Nyamu alisema.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kauli hii inajiri siku moja tu baada ya vyanzo vya habari humu nchini kudai kwamba mali ya Karen Nyamu huenda ikawekwa kwenye soko la mnada baada ya kukosa kulipa kodi ya nyumba.

Inaripotiwa kwamba Nyamu anadaiwa kodi ya nyumba ya hadi shilingi milioni 1.25 na mwenye nyumba wake.

Hata hivyo, Nyamu akizungumza katika kituo kimoja cha runinga humu nchini Jumanne, alipuuzilia mbali madai hayo akisema kwamba yeye na mwenye nyumba wake wako katika maelewana mazuri.

Pia alifichua kuwa baadhi ya watu wanatumia mbinu za siri kujaribu kumshinikiza afanye mambo ambayo hakutaja.

"Kuna watu wanaofikiri wanaweza kufadhili vyombo vya habari, kutumia njia za kihuni kukupotosha na kukutisha, na kwenda kwenye matakwa ili kutoa ahadi ambazo wanajua kabisa si sahihi," alisema.

Alifunga mjadala, na kuongeza kuwa hayuko tayari kushughulikia maswala yake hadharani.

"Na niko hapa kuwafundisha haifanyi kazi na kila mtu. Njia sahihi lazima ifuatwe na sitaki kushughulikia masuala yangu hadharani,” alisisitiza.

Nyamu hata hivyo alifichua kwamba baada ya ripoti za kudaiwa kodi ya nyumba kusambaa, alipokea hela kadhaa kwenye simu yake kutoka kwa watu lakini akasema hahitaji michango zaidi.

"Kwa kweli nilipata michango kwenye simu yangu na ninashukuru Wakenya lakini sijambo, sihitaji michango sasa."