Seneta maarufu wa kuteuliwa Karen Njeri Nyamu ameahidi kutoa ufafanuzi wa kina kufuatia tetesi kuwa madalali wanalenga kuuza vitu vyake vya nyumbani kwa madai ya malimbikizo ya kodi.

Katika ujumbe wa X siku ya Jumatatu, mama huyo wa watoto watatu alikejeli hali hiyo akisema kuwa baadhi ya watu wa karibu walikuwa wameeleza wasiwasi wao kufuatia uvumi huo wa kushtua.

Alisimulia jinsi mwenzake mmoja alivyomwendea akitaka kujua alikokuwa akipeleka pesa zake ikiwa hakuwa anaweza kulipa kodi kama ilivyodaiwa.

“Unajua kwanini nacheka. Kuna mwenzangu ameniuliza akiwa na wasiwasi sana kama nimekuwa mraibu wa kamari ya casino?? Ati pesa inaenda wapi,” Karen Nyamu aliandika kwenye mtandao wa X.

"Tulia nitawapigia story," aliongeza.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Hii ilikuwa baada ya ripoti kuibuka kuwa madalali wanafuatilia vitu vya nyumbani vya mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata kuhusu madai ya malimbikizo ya kodi ya Ksh1.25milioni.

Siku ya Jumatatu, iliripotiwa kuwa, amri ya mahakama iliyotolewa na Hakimu Mwandamizi wa Milimani A.H. Nyoike mnamo Novemba 13, 2024, ilionyesha kuwa seneta Nyamu yuko hatarini kupigwa mnada ili kurejesha kiasi cha kodi ambacho hakijalipwa.

Kulingana na amri ya korti, kiasi hicho kingerejeshwa na Fantasy Auctioneers kwa niaba ya mwenye nyumba.

Mahakama pia iliagiza Kituo cha Polisi cha Runda kuweka ulinzi kwa madalali hao.

"Ofisa anayesimamia Kituo cha Polisi cha Runda au afisa mwingine yeyote aliye chini ya amri yake atoe msaada kwa madhumuni ya kudumisha sheria na utulivu," ilisomeka amri ya mahakama.

Seneta Nyamu hata hivyo amepinga hatua ya vitu vyake vya nyumbani kupigwa mnada.

Vitu vilivyolengwa viko nyumbani kwa mwanasiasa huyo katika Graceville Villas, mtaa wa Runda.