MFANYIBIASHARA Niffer ambaye ni rafiki wa karibu wa msanii Alikiba ameripotiwa kutiwa mbaroni na jeshi la polisi Tanzania baada ya kudaiwa kuchangisha pesa za kuwasaidia wahanga wa jengo lililoporomoka Kariakoo sokoni.

Hii ni baada ya waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kutoa amri ya kukamatwa kwa mrembo huyo kwa kile alisema anachangisha hela za msaada bila utaratibu mwafaka.

Majaliwa alitoa amri ya kukamatwa kwake wakati alifanya ziara ya ghafla katika eneo la mkasa ambapo jengo la ghorofa 4 liliporomoka siku chache zilizopita.

“Yuko binti ambaye anaitwa Niffer, mumeona anasema anachangisha na nimeona mpaka jana alisema amekusanya zaidi ya milioni 37, atafutwe! Kwanza atuambie nani alimpa kibali cha kuchangisha. Utaratibu huu wa kuingiza pesa kwa simu yake alipata kibali wapi? Na amekusanya shilingi ngapi? Anasema ananunua maziwa, ameyapeleka wapi?” Waziri mkuu alihoji.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Waziri mkuu huyo alithibitishiwa kwamba Niffer tayari alikuwa amewekwa chini ya ulinzi na kuwataka kumhoji na kufunga ile akaunti aliyokuwa akitumia kuchangisha pesa.

Kiongozi huyo pia alitumia kisa cha Niffer kama mfano kutoa onyo kwa mwananchi yeyote wa taifa hilo dhidi ya kutumia fursa ya mkasa wa kuporomoka kwa jengo la Kariakoo kuchangisha pesa bila idhini ya mamlaka husika.

“Kwa kuwa mmeshampata, mhoji na mhakikishe kwamba mmefunga ile akaunti. Na kupitia tangazo hili, haturuhusu mtu yeyote kujitoa kusimamia michango ya watu kwa ajili ya hapa,” Majaliwa alisema.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mikasa kama ule wa Kariakoo upo chini ya wizara ya waziri mkuu, kitengo cha maafa. Katika kitengo hicho, kuna sheria iliyopitishwa mwaka 2022 inayoratibu jinsi maafa kama hayo yanashughulikiwa.

Wakili mmoja alieleza kwamba Niffer alifanya kosa chini ya kifungu namba 36(2) cha sheria hiyo ya maafa ambacho kinasema kwamba mtu yeyote atakayekusanya pesa za maafa bila kuwasilisha kwenye kamati ya maafa, atakuwa amefanya kosa na adhabu yake ni kifungo cha kati ya mwaka mmoja hadi miaka 5 jela au kulipa mara mbili ya fedha ambazo itabainika amezikusanya au yote mawili.