Jimbo Kuu la Katoliki la Nairobi limekataa michango ya pesa ya wanasiasa.
Katika barua iliyofikia Radio Jambo na kutiwa saini na Askofu Mkuu Philip Anyolo, uongozi wa kanisa hilo umekataa mchango wa pesa uliotolewa kwa kanisa na Rais William Ruto na Gavana wa Nairobi Jonson Sakaja wikendi iliyopita.
Siku ya Jumapili, Rais Ruto alihudhuria ibada katika Kanisa la Katoliki la Soweto jijini Nairobi, akiandamana na Gavana wa Nairobi Sakaja.
Katika barua hiyo, Dayosisi ya Nairobi ilisema Ruto alitoa mchango wa Sh600,000 kwa kwaya ya Kanisa la Katoliki la Soweto na mishonari ya parokia hiyo, huku Gavana Sakaja akichangia Sh200,000.
Rais pia alitoa mchango wa Sh2 milioni za ujenzi wa nyumba ya Baba na aliahidi kulizawadi kanisa hilo basi mnamo Januari mwaka ujao.
Hata hivyo, katika barua ambayo kanisa hilo lilichapisha mtandaoni, Askofu Mkuu Anyolo alisema kuwa Kanisa la Nairobi litadumisha msimamo thabiti kuhusu michango ya wanasiasa, akiangazia hitaji la Kanisa kujilinda dhidi ya kutumiwa kwa malengo ya kisiasa.
"Fedha hizi zitarejeshwa kwa wafadhili husika. Aidha, Sh3 milioni zilizoahidiwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Baba pamoja na michango ya basi la parokia kutoka kwa rais zinakataliwa," inasomeka sehemu ya barua hiyo.
Katika barua hiyo, Anyolo analishauri kanisa kudumisha uadilifu na kukataa michango ambayo inaweza kuhatarisha uhuru wake bila kukusudia.
"Wanasiasa wanashauriwa kuonyesha uongozi wa kimaadili kwa kushughulikia masuala muhimu yaliyoibuliwa na KCCB. Kanisa lazima lisalie kuwa chombo kisichoegemea upande wowote bila ushawishi wa kisiasa ili kutumika kikamilifu kama nafasi ya ukuaji wa kiroho na mwongozo wa jamii,” barua hiyo inasomeka kwa sehemu.
Alhamisi wiki jana, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB) lilidai kuwa kuendelea kutoza ushuru mpya kwa Wakenya ni njia ya siri ya kuwasilisha tena Mswada wa Fedha uliokataliwa.
Huku wakikiri kwamba serikali inaweza tu kuongeza mapato yake kupitia kodi, maaskofu walisikitika kwamba raia walikuwa wanatozwa ushuru kupita kiasi.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!