
MSANII na mjasiriamali wa vyombo vya habari, Alikiba
ni miongoni mwa waokoaji kadhaa ambao wamejitokeza na kujitosa kimasomaso ndani
ya vifusi vya jengo lililoporomoka jijini Dar es S alaam kutoa msaada wa uokoaji.
Mkurugenzi huyo wa Crown Media na Kings Music
alijumuika na waokoaji wengine usiku wa Jumatatu akiwa amevalia mawanda ya
uokoaji.
Alikiba alionekana akizama ndani ya vifusi vya jengo
hilo la orofa nne lililoporomoka siku chache zilizopita katika soko kuu la
Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Baada ya kufika ndani ya vifusi hivyo ambapo shughuli
ya uokoaji imekuwa ikiendelea kwa mwendo wa kujikokota kwa zaidi ya siku 3
sasa, alisema kwamba ni jambo la kusikitisha lakini pia akawapongeza wote ambao
wanakesha usiku na mchana kuhakikisha wenzao walionaswa ndani ya vifusi hivyo
wanaondolewa, ima hai au wakiwa wamefariki.
“Kwa
nafasi yangu mimi nimeweza kufika katika eneo la tukio na kiukweli kazi
inayoendelea hapa ni kubwa sana, na kuna vitu vya kusikitisha lakini vile vile
kuna vitu vya kuwapongeza baadhi ya wale wanaofanya kazi kubwa ya uokoaji,”
Alikiba alisema.
Aliipongeza serikali ya Samia Suluhu Hassan kwa kile
alisema kwamba japo walichelewa, lakini waliweza kufanikisha kuleta wataalamu
wa kufanya jambo la kuchimba vifusi ili kuokoa maisha.
“Wananchi
ndio kila mmoja ameumizwa na kuguswa na jambo hili lakini hili si jambo la
kukurupuka useme unatumia nguvu. Hili linaitaji utaalamu. Kama hatuna elimu ya
uokoaji kwa jinsi hili jengo lilivyokaa tutajikuta tunaumiza wengine kwa sababu
kuna wengine wapo chini na wanawasiliana na waokoaji.”
Msanii huyo aliwaomba watumizi wa mitandao ya kijamii
kupunguza mizaha kuhusu kuporomoka kwa jengo hilo, akisema kwamba mwenyewe
ameingia hadi ndani kabisa ya jengo la kushuhudia hali ilivyo tete kwa wale
walionaswa.
“Kiukweli hili si jambo la kufanyia mzaha tena kwenye
mitandao kama inavyoongeleka. Kuna watu wanaongea taarifa tofauti lakini hapa
kluna uangalizi mkubwa sana. Hapa kuna usalama mkubwa umewekwa kiasi kwamba
hata ufikaji wangu mimi imekuwa ni mchakato mrefu,’ alisema.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari kutoka nchini humo,
kufikia Jumatatu, takribani watu 13 walithibitishwa kufariki katika mkasa huo
ambao umetajwa kuwa mbaya na rais Samia Hassan.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!