
Mwanasosholaiti Huddah Monroe amemmiminia sifa mbunge
wa Embakasi Mashariki, Paul Ongili maarufu kama Babu Owino, akifichua kuwa
ndiye chanzo cha utajiri alio nao kwa sasa.
Monroe alichapisha msururu wa jumbe za kumvisha koja
la maua Babu Owino akisema kuwa ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kumtoa mitaani na
kumuonyesha njia za kutafuta pesa.
Huddah alisimulia kwamba alikuwa ni maskini wa
kutupwa hadi wakati alipokutana na Babu Owino ambaye alimshika mkono na
kumuonyesha jinsi ya kutafuta pesa na utajiri.
“Nilikuwa
nikihangaika, yaani sikujua kodi inayofuata ingetoka wapi. Sijui ni jinsi gani
au ni nani aliyenitambulisha kwa Babu Owino enzi hizo. Niliishi kwenye nyumba
ya chumba kimoja hapo Kile. Barabara ya
Kandara.”
“Babu
ananipigia simu siku moja, ananichukua kwenye Benz! Ndio jamaa alikuwa na Benz
siku hizo. Nadhani aliweza kusema kuwa nilikuwa najitahidi kweli! Akaniuliza
‘umechoka kuishi mkono kwa mdomo?’ Je, hata mimi nilikuwa naishi? Tuliendesha
gari karibu na Arboretum na akanionyesha jinsi ya kutengeneza sarafu! Mengine
ni historia! Lakini alifungua macho yangu ya umaskini,”
Huddah alisimulia.
Mrembo huyo ambaye siku za hivi karibuni ameonekana
kuwa mstari wa mbele kuzungumzia hali ya uchumi wa Kenya chini ya utawala wa
rais William Ruto, alisema hata hivyo urafiki wake wa muda mrefu na Babu Owino
ulikatika miaka michache iliyopita.
Huddah alifichua kwamba alianza kumuona Babu Owino
kwa taswira tofauti baada ya kuhusishwa na tukio la kumfyatulia risasi mcheza
santuri DJ Evolve katika klabu moja ya starehe mtaani Kilimani miaka michache
iliyopita.
Huddah alisema kwamba hajui tukio hilo alilaumu kwa
Babu Owino au kwa ulevi.
“Tulikosana
alipompiga risasi yule kijana labda ilikuwa pombe, kusema kweli maji ya
mashetani yanaweza kukupelekea kufanya dhambi za kichaa. Lakini ndani ya roho
yake, Babu Owino ni mtu mzuri. Hataona vijana wakihangaika wala jiji likigeuka
kuwa makazi duni na anyamaze,” Huddah alimpaisha Babu.
Babu Owino, mtetezi mkali wa sera za chama cha ODM
amekuwa akihusishwa kujitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana katika kaunti ya
Nairobi mwaka 2027 ambapo huenda akamenyana na gavana wa sasa, Johnson Sakaja.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!