Mchekeshaji na muigizaji Dj Shiti ameibuka na utani kuhusu  kitu ambacho kimekuwa kikimnyima usingizi tangu wiki hii ilipoanza.

Kupitia Instagram, Shiti alikiri kwamba amekuwa akifikiria siku nzima hadi kupata msongo wa mawazo akijaribu kufikiria kuhusu pazia atakazotumia msanii Khaligraph Jones katika jumba lake kubwa.

Shiti alisema kwamba kila wakati anapojaribu kuketi chini na kutulia, anajipata akitafakari kiwango cha pazia ambazo rapa huyo wa ‘Mazishi’ atakuwa akishonewa ili kutoshea katika madirisha ya jumba lake la kipekee.

Na imagine khaligraph atashonesha Curtains kiasi ganiii ?? hiyo kitu imeni Stress the whole day,” Shiti aliandika katika picha yake akiwa ameshika kidevu akiwa amekalia kiti kidogo.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Msanii Khaligraph Jones amekuwa gumzo la mitandao ya kijamii kwa takribani siku 3 sasa baada ya kuonyesha picha na video za jumba lake kubwa ambalo limezua mjadala mitandaoni.

Baadhi ya watumizi wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakitania jumba hilo wakilifananisha na jumba la biashara za jumla, huku wengine wakilifananisha na jumba la masomo ya chuo kikuu.

Hata hivyo, Jones alijitokeza akisema kwamba maoni ya watu kuhusu jumba lake hayamnyimi usingizi hata kidogo, akiweka wazi kwamba shida kama hizo ndizo alikuwa akiomba zimfuate kwa muda mwingi.

"Unaamka unapata unatrend sababu umejenga nyumba kubwa inakaa kama maduka, Mungu anajua haya ndio matatizo niliyokuwa natamani," Khaligraph alisema.

Awali, alidokeza kwamba muundo wa jumba lake huenda umechochewa na maisha ya kisanii ya rapa wa Marekani, Rick Ross ambaye pia anamiliki jumba la kipekee nchini Marekani.

Jones alisema kwamba kwa wale ambao hawajafika kwake, wajue kwamba madhari yenyewe ni kama mtu kuingia Marekani kwa jumba la Rick Ross.

Alionekana kutupa kijembe kwa wakosoaji wa jumba lake akisema watu wengi hawajazoea majumba ya muundo huo na ndio wanaobwabwaja kwenye mitandao ya kijamii.

“Hamjazoea hizi settings, hapa ukikuja ni kama umeingia Amerika, kwa Rick Ross. Heshima ni lazima kwa OG,” Khaligraph Jones alisema huku akicheka.

Siku ya Jumatatu, Jones alishangazwa na watu ambao walikuwa wanachapisha picha na video za jumba lake mitandaoni wakiambatanisha na kauli za dharau kuhusu mjengo huo.