
Msanii wa rap ya kiazi kipya ambaye pia ni mtengenezaji maudhui ya kuchekesha, Stevo Simple Boy ametangaza sherehe yake kubwa itakayofanyika mwezi ujao kuadhimisha miaka 5 tangu alipojiunga kwenye Sanaa ya muziki nchini.
Simple Boy ameweka tangazo hilo wazi kupitia klipu fupi kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo ametangaza eneo litakaloandaa tamasha hilo pamoja na viingilio.
Stevo alisema kwamba mapema mwezi ujao, atakuwa anaadhimisha miaka 5 ya kuwaburudisha Wakenya si tu kwa muziki bali pia kwa kauli changamano zenye vichekesho na mtindo wake wa uvaaji.
“Wananiita Stevo Simple Boy, mzee wa matulinga ambaye watu wanampenda kila siku. Tarehe 6 Desemba mjini Kisii mambo yatachemka, sherehe itakuwa kubwa. Itakuwa ni Stevo @5, anasherehekea miaka kwenye Sanaa ya muziki,” alisema akiwa na watengeneza maudhui wengine kutoka Kisii.
Akitangaza kiingilio, Stevo alisema kwamba watu watapata burudani kuanzia shilingi 500 pekee.
“Kiingilio ni shilingi 500 kwa sehemu za kawaida, VIP ni 2,000 na VVIP ni 5,00 peke yake.”
Msanii huyo alijizolea umaarufu kwenye Sanaa ya muziki mwaka 2019 na kibao chake cha kwanza cha ‘Mihadarati’.
Tangu wakati huo, Simple Boy ameachilia vibao vingine kadhaa vilivyowavutia Wakenya, kama vile ‘Tuheshimu Ndoa, Freshi Barida, Mafi Mafi Mushkla, Shega’ miongoni mwa ngoma nyingine.
Utunzi wa msanii huyo kutoka Kibera ni wa kipekee kwani anaimba kwa kutumia misemo na kauli zenye kuchekesha ambazo mwisho wa siku hugeuzwa kama meme mitandaoni.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!