Afisa mkuu mtendaji wa MCSK, Dkt Ezekiel Mutua amewashauri wasanii wa Kenya kuzingatia unyenyekevu wakati nyota yao inapong’aa na kuwakweza hadi kileleni.


Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mutua alitoa wosia huo akiwashauri wasanii dhidi ya kutingiwa na kiburi na majivuno pindi wanapopata umaarufu na majina yao kuwa tajika.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans


Kwa mujibu wa Mutua, wasanii na watu wengi maarufu wanaporomoka baada ya muda mfupi kutokana na kuingiwa na ustaa unaowafanya kuanza kuwaona mashabiki wao kama kinyaa.


“Kwa wasanii wetu, Wakati nyota yako inang'aa na wewe ni jina kubwa, kuwa mnyenyekevu. Ni muhimu kudumisha unyenyekevu na uadilifu. Wakati chapa yako iko katika kilele na unapata gigs kila mahali, wakati mashabiki wako wanakupenda sana na kuonyesha uabudu wa kipekee, usichukuliwe na umaarufu na kuwa wazembe,” Mutua alishauri.


Mutua pia aliwakanya wasanii dhidi ya kukubaliwa kutumia kiki ili kusukuma mambo yao, akisema kwamba kiki huenda ikawasaidia kwa muda mfupi lakini ikaharibu kabisa taaluma yao kwa maisha.


“Zingatia mambo unayosema au kuchapisha kwenye mitandao ya kijamii. Unaweza kuharibu chapa yako kwa kukimbiza kiki na kujivunia basi mashabiki hao hao watakugeukia na kukuepuka kama tauni. Tafuta ushauri na uwe na wasimamizi wanaowajibika na waliokomaa ambao wanaweza kukuongoza kutumia ushawishi wako vyema,” Mutua alitema lulu.


Wasanii wengi wa Kenya wamekuwa wakijipata katika hali ngumu kubaki katika umaarufu kwa zaidi ya miaka miwili baada ya kupata umaarufu.