Watu takriban 25 wameuawa katika mlipuko wa bomu kwenye stesheni ya treni katika jimbo la Balochistani, nchini Pakistani.
Makumi ya watu wengine wamejeruhiwa kufuatia mlipuko huo uliotokea wakati treni yenye abiria wengi ya asubuhi ilipokuwa ikijiandaa kuondoka kwenye stesheni ya Quetta.
Kundi la wanamgambo la Balochistan Liberation Army, limekiri kutekeleza shambulio hilo ambalo tathmini ya polisi inaonesha lilikuwa ni la kujitoa mhanga.
Kumeshuhudiwa ongezeko na mashambulizi katika jimbo hilo katika siku za hivi karibuni. Kundi hilo linapigania uhuru na udhibiti wa rasilimali wa jimbo hilo.
Kwa mujibu wa kamishna wa jiji, watu 25, akiwemo aliyejitoa mhanga, waliuawa katika mlipuko huku takribani watu 50 wakijeruhiwa.
Afisa mwandamizi wa polisi Muhammad Baloch amesema inashukiwa kuwa aliyejitoa mhanga alivaa vilipuzi vyenye kilo baina ya sita mpaka nane.
Raia wa kawaida na wanajeshi ni miongoni mwa watu waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo, afisa huyo ameiambia BBC
Video zilizochapishwa mitandaoni zinaonesha wakati mlipuko huo ukitokea mapema asubuhi ya leo, huku kukiwa na makumi ya watu wakiwa katika harakati za kuabiri treni.
Abdul Jabbar ni miongoni mwa majeruhi waliofikishwa katika Hospitali ya Kiraia. Alisema kuwa alikuwa akiingia kituoni, akiwa amenunua tikiti kutoka kwa ofisi ya uhifadhi, mlipuko ulipotokea.
"Siwezi kuelezea hofu niliyokumbana nayo leo, ilikuwa kana kwamba siku ya hukumu imefika," alisema
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!