Mshukiwa mkuu wa mauaji ya mtangazaji wa redio Lilian Aluko alikamatwa siku ya Ijumaa baada ya kuwa mafichoni kwa siku kadhaa.

George Mwenda Mutegi, ambaye alikuwa mpenzi wa marehemu, alipatikana katika maficho yake katika eneo la Kaanwa, Kaunti ya Tharaka Nithi kufuatia msako mkali wa timu ya maafisa kutoka makao makuu ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na maafisa wa usalama katika eneo la Meru.

Kulingana na DCI, msako wa kumtafuta Mutegi ulianza Novemba 1, 2024, usiku ambao inaaminika mshukiwa alimuua mwanahabari huyo mpenziwe.

"Baada ya mauaji hayo ya kinyama, Mutegi alitoweka na kufuta nyayo zake," DCI walisema kwenye taarifa.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Marehemu Aluko aliuawa mnamo Novemba 1. Mwili wake usio na uhai ulipatikana ukiwa umelowa damu ukiwa na ukiwa na jeraha la kisu nyuma ya sikio la kulia na majeraha yanayoonekana usoni na kwenye nyonga.

Maafisa wa polisi wanaochunguza kisa hicho waligundua kuwa wapenzi hao wawili walikuwa na wakati mzuri kwenye eneo moja la burudani, kabla ya kuelekea kwenye nyumba ya Mutegi katika eneo la Kahawa West.

Punde si punde, umakini wa majirani ilivutwa na mayowe makubwa kutoka kwa nyumba ya Mutegi iliyokuwa imefungwa. Mayowe hayo hata hivyo yalifunikwa haraka na kelele kubwa kutoka kwa redio yake. 

Bila kujua kwamba kilio hicho kilikuwa cha mwisho kabisa ambacho Achieng angeweza kufanya, majirani walirudi nyumbani kwao wakitumaini kwamba wawili hao wangetatua masuala yao.

Usiku huo, maisha ya mwanadada huyo mrembo mwenye umri wa miaka 33 ambaye taaluma yake ya utangazaji wa redio ilikuwa ikinawiri yalikatishwa. 

DCI wameripoti kuwa mshukiwa huyo kwa sasa anashikiliwa katika kituo cha polisi kabla ya kufikishwa mahakamani huku maafisa wakiendelea kuchunguza kisa hicho ili kujua kilichojiri.