Rapa mkongwe wa Kenya Hubert Mbuku Nakitare almaarufu Nonini ametishia kumchukulia hatua ya kisheria mtumiaji mwingine wa mtandao kwa madai ya kumchafulia jina.
Siku ya Alhamisi, rapa huyo ambaye kwa sasa anaishi Marekani na familia yake, kupitia mawakili wake alituma barua ya madai kwa mtumiaji wa mtandao wa kijamii wa X Hussein Mohammed almaarufu @Saddam_KE kwa madai kwamba alichafua jina lake.
Katika barua hiyo, Nonini alidai kuwa Bw Hussein, katika tweet ambayo alichapisha mnamo Novemba 6 alitoa matamshi ya uongo dhidi yake akimtaja kama tapeli.
“Tumeelekezwa kuwa kutokana na taarifa yako ulidokeza kuwa mteja wetu ni tapeli na anaishi New York Marekani. Kwamba zaidi, wakati Donald Trump anaingia madarakani kama Rais wa 47 wa Marekani, inambidi kuishi kulingana na msemo wake ‘MAKE AMERICA GREAT AGAIN’ maarufu kwa jina la MAGA' na ili kufikia hili, inambidi kumrudisha mteja wetu NONINI nchini Kenya kutokana na njia zake za uhalifu,” barua iliyotiwa saini na wakili Katee David ilisoma.
Katika barua hiyo, mwanzilishi huyo wa lebo ya muziki ya PRO-HABO pia alibainisha kuwa hajui sababu zinazomfanya mwanamtandao huyo kuendelea kumshambulia licha ya kuwa hawajawahi kukutana wala kuzungumza hapo awali.
Pia alisema kwamba awali alichagua kupuuza mashambulizi ya Saddam hadi alipodaiwa kuchapisha matamshi ya kashfa ambayo yalijizolea maelfu ya watazamaji.
"Taarifa iliyotumwa na wewe mwenyewe imeenda mbali zaidi na kufikia familia ya wateja wetu, marafiki na washirika wa biashara ambao baadhi yao wamefika kwake ili kuuliza kuhusu madai yako. Kauli yako ya uwongo na kashfa na unyanyasaji unaoendelea mtandaoni umemsababishia mteja wetu uchungu wa kiakili na tunaweza kuthibitisha kwamba ametupa ushahidi wote ikiwa ni pamoja na rekodi za sauti na picha za mahojiano ambayo umehudhuria na kuliburuza jina lake tope bila sababu za msingi. ,” barua hiyo ilisomeka.
Kutokana na hayo, mawakili wa Nonini wamemwagiza mwanamitandao huyo kufuta tweet aliyoweka kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X na pia kuomba msamaha ndani ya saa 24 baada ya kupokea barua hiyo.
Mapema wiki hii, mtumiaji wa X @Saddam_KE aliposti ujumbe wa Twitter akimsihi rais anayekuja wa Marekani kumfukuza nchini tapeli ambaye anadaiwa kuwa anaishi New York. Alidai kuwa tapeli huyo amekuwa akijifanya kuwa rapa na akabainisha kuwa anaitwa Nonini.
Katika tweet nyingine, Saddam hata hivyo alidai kuwa alikuwa akimrejelea rapper wa Marekani Lil Wayne.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!