Makamu wa rais wa Marekani anayeondoka madarakani na ambaye alikuwa mgombea urais wa Chama cha Democratic Kamala Harris amekubali kushindwa katika uchaguzi wa urais uliomalizika hivi punde.
Trump alichaguliwa kuwa rais wa 47 wa Marekani siku ya Jumatano, katika hali ya kushangaza kwa rais huyo wa zamani ambaye alikataa kukubali kushindwa takriban miaka minne iliyopita.
Katika taarifa yake usiku wa kuamkia Alhamisi, Harris ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Trump katika uchaguzi wa 2024 alibainisha kwamba anakubali matokeo ya upigaji kura, licha ya kuwa si jinsi yeye na wafuasi wake walivyotaka.
"Moyo wangu umejaa leo- umejaa shukrani kwa imani mliyoweka kwangu, iliyojaa upendo kwa nchi yetu, na kamili ya azimio. Matokeo ya uchaguzi huu sio yale tuliyotaka, sio yale tuliyopigania, lakini nisikie ninaposema: nuru ya ahadi ya Amerika itawaka kila wakati," Harris alisema katika taarifa.
Mwanasiasa huyo aliendelea kufichua kuwa tayari alipiga simu kwa Trump kumpongeza na kuahidi kumuunga mkono yeye na timu yake.
“Lazima tukubali matokeo ya uchaguzi huu. Mapema leo, nilizungumza na Rais Trump na kumpongeza kwa ushindi wake. Nilimwambia kwamba tutamsaidia yeye na timu yake katika mabadiliko hayo, na tutashiriki katika uhamisho wa amani wa mamlaka,” aliongeza.
Rais anayeondoka wa nchi hiyo, Joe Biden pia alimpigia simu Trump kumpongeza na kumwalika rais mteule huyo kwenye Ikulu ya White House, akianzisha rasmi kipindi cha mpito kabla ya Siku ya Kuapishwa, Ikulu ya Marekani ilisema.
Biden pia alimpigia simu Harris kumfariji.
Viongozi wengi wa Mataifa ya Kigeni walimpigia simu Trump pia kumpongeza, akiwemo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!