Seneta wa kaunti ya Migori Eddy Oketch amemwandikia spika Amason Kingi akiomba kufanyika kwa uchunguzi wa kina kuhusu madai ya kampuni ya mawasiliano ya Safaricom kudaiwa kuvujisha data za kibinafsi za wateja wao kwa DCI.

Katika barua yake, Oketch ambaye pia alizungumzia suala hilo kwenye seneti Alhamisi alisema kwamba ni ukiukwaji mkubwa wa sheria kwa kampuni kutoa maelezo ya kibinafsi ya wateja wake bila idhini yao.

“Ningependa kupata taarifa kutoka kwa kamati inayiosimamia mawasiliano na teknolojia kuhusu madai ya ukiukaji wa kutolewa kwa maelezo ya kibinafsi ya wateja wa Safaricom,’ Oketch alimsomea spika Kingi barua yake.

“Bwana Spika katika taarifa, kamati hiyo inastahili kubaini kama katika miaka 4 iliyopita, Wakenya wamewahi toa malalamiko kuhusu Safaricom kuvujisha data zao na kuonyesha hatua zilizochukuliwa..’ Oketch aliongeza.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Pia alitaka kamati hiyo kufanya uchunguzi kubaini iwapo Safaricom wana maelewano na baadhi ya idara za serikali kuhusu kuwapa data na maelezo ya kibinafsi ya wateja wao.

Katika barua hiyo yenye matakwa 7, Oketch aliomba pia uchunguzi kufanyika kubaini iwapo Safaricom ina idhini ya kukusanya na kuweka maelezo ya kibinafsi ya wateja wake, kama vile kuonyesha sehemu walipo na kufuatilia wanachozungumza kwenye simu.

Madai haya yanajiri siku chache baada ya jarida moja la humu nchini kueleza kuwa Safaricom ilipachika Neural Technologies, mfumo wa usimamizi wa data katika mifumo yake ya ndani inayoruhusu huduma za usalama bila vikwazo kwa ufikiaji wa wakati halisi wa data ya simu za Wakenya, madai ambayo Safaricom ilikanusha.

Siku ya Jumatano, Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai, DCI pia alikanusha madai hayo, akisema polisi wanategemea tu watoa huduma za simu kwa asilimia ndogo ya uchunguzi wao.

“Kuhusu suala la polisi kula njama na watoa huduma za simu, hatufanyi hivyo kabisa, ikiwa tuna nia ya kupata taarifa kutoka kwa watoa huduma tunafanya hivyo kwa njia halali. Tunaenda kwa mahakama, kuapa hati za kiapo, na kutoa amri hiyo kwa watoa huduma” alisema Mohamed Amin.