Rais William Ruto ameonyesha Imani yake kwa naibu wake mpya Kithure Kindiki kuweza kutekeleza yale ambayo yameshindwa kutekelezwa na afisi ya naibu rais katika kipindi cha miaka 2 iliyopita.

Akizungumza pindi baada ya kuapishwa kwa Kindiki katika ukumbi wa KICC, Ruto alimuomba Kindiki kuleta sauti na ujuzi wake mezani kwa ajili ya kufanikisha malengo ya serikali yake.

Rais Ruto alifichua kwamba katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, alikuwa sauti ya pekee kwenye uongozi wake kunadi miradi inayotekelezwa na serikali bila kusaidiwa na naibu wake aliyebanduliwa, Rigathi Gachagua.

Kiongozi wa taifa alimuomba Kindiki kumsaidia kunadi miradi hiyo kwa wananchi, akionyesha Imani yake kwamba anamfahamu kuwa ni mtu mwenye akili na ujuzi utakaosaidia serikali kutimiza ahadi zake kwa wapiga kura wake.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Profesa Kindiki, nahitaji sauti yako, nahitaji akili na ujuzi wako kunisaidia na kusaidia wananchama katika baraza letu la mawaziri kuorodhesha miradi ambayo tunafanya na kuzungumza kuhusu vitu ambavyo tunavifanya,’ Ruto alisema.

“Nimekuwa karibia sauti pweke haswa kwenye uongozi wetu kuzungumzia na kuelezea kuhusu miradi na mipango yetu. Wewe ni fasaha kaka yangu, wewe ni mwerevu na nina Imani kwamba utafanya yale ambayo nimekosa kufanyiwa kwa miaka miwili iliyopita. Najua unaweza,” Ruto aliongeza.

Kindiki aliapishwa mapema Ijumaa katika hafla ya mbwembwe na shangwe iliyofanyika katika ukumbi wa KICC na kuhudhuriwa na rais na viongozi wengine serikalini.

Hafla hiyo ilidumu kwa takribani saa moja na nusu kabla ya rais kuondoka na naibu wake mpya.

Kindiki anachukua nafasi ya Rigathi Gachagua aliyebanduliwa ofisini na seneti wiki mbili zilizopita baada ya kudaiwa kujipatia mali kwa njia za kifisadi pamoja na kutelekeza majukumu yake, miongoni mwa mashtaka mengine.