Rais William Ruto ametoa rai ya kipekee kwa Wakenya akiwaomba kukoma kuamini katika habari za kupotosha na propaganda kuhusu uongozi wake.

Akizungumza Gilgil wakati wa kufuzu kwa maafisa wa huduma ya misitu, KFS, Ruto aliwataka Wakenya kutotilia maanami habari feki zinazoenezwa mitandaoni kwamba Kenya imedorora kiuchumi katika miaka miwili iliyopita tangu alipokabidhiwa mamlaka ya kuwa rais.

Alifafanua kwamba ukweli upo kuwa Kenya imeimarika kwa kasi kubwa katika kipindi cha miaka 2 iliyopita, akisema kuwa propaganda zinazoelezea vinginevyo zinaumiza taifa hili zuri.

“Sisi sote, kama watu wa Kenya, ni wakati wa kuamini katika nchi hii kuu ambayo Mungu ametupa. Umefika wakati wa kuacha negativity na kuacha kuamini habari za uongo na propaganda zinazoliumiza taifa letu. Mabadiliko yamekuwa ya ajabu katika miaka miwili iliyopita,” alisema.

Rais Ruto alizungumza katika Chuo cha NYS huko Gilgil, Kaunti ya Nakuru, ambapo aliongoza hafla ya kufuzu kwa maafisa 574 wa misitu. Rais alitolea mfano kazi ambayo imetekelezwa na KFS katika kipindi cha miaka miwili akisema, wamefanya kazi ya kupendeza kuzuia ukataji vovyo wa miti na kuharibiwa kwa misitu.

“Ambacho kimefanikiwa katika kipindi cha miaka miwili, kwa kupunguzwa mambo haramu misituni kwa asilimia 90 ni jambo ambalo tunafaa kujivunia. Ukweli kwamba KFS sasa wanaweza kupata rasilimali zao wenyewe kwa sababu ya mabadiliko na mageuzi ambayo yamefanyika, ni jambo ambalo tunastahili kusherehekea,” aliongeza.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Maafisa hao wakiwemo Wakada wa Wakaguzi wa Huduma za Misitu na Wakufunzi wa Misitu walihitimu mafunzo hayo baada ya kumaliza mafunzo ya miezi sita ya Utekelezaji wa Sheria ya Misitu na mwezi mmoja wa mafunzo ya mbinu katika mazingira magumu na machafu ya misitu.