
“Ningependa kuwaambia, enyewe ni kama kuomba msamaha. Nimekaa nje kwa miaka mingi, sasa wanisamehe nikae nyumbani. Sasa nilienda tu hivyo na nikashindwa hata ningerudi singejua nyumbani ni wapi,” Nyaanga alisema kwa sauti ya majuto.
Mzee huyo kwa jina Joseph Nyaanga, mwenye umri wa miaka 70 kutoka eneobunge la Bonchari kaunti ya Kisii alirejeshwa nyumbani baada ya kuviziwa katika kaunti ya Baringo alikokuwa.
Nyaanga alikiri kwamba alipotoka nyumbani miaka 34 iliyopita kuenda kutafutia familia yake riziki, alizama kwenye riziki na kusahau njia ya kurudi nyumbani ambapo alitia nanga Baringo na kuanzisha maisha mapya na familia nyingine.
“Kutoka kwangu nyumbani, ni hii kazi tulikuwa tunafanya ya barabara na kujenga daraja. Ndio kazi ilinitoa nyumbani. Nikaenda mpaka nikajikuta nimesahau,” mzee huyo aliiambia runinga ya Citizen.
Akiwa katika kaunti ya Baringo, mzee huyo alipata watoto 7 na mke mpya na kufanya idadi ya wanawe wote kuwa 10, ukiongeza na wale 3 alioacha na mke wa kwanza Kisii miaka 34 iliyopita.
Mzee huyo alitoka nyumbani mwaka wa 1990 na baada ya kurejea kwake, aliomba radhi kwa jamaa zake akiahidi kuanza upya baada ya kujikwaa katika kutekeleza majukumu yake kama baba wa familia.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!