Akizungumza kwenye mahojiano katika kituo cha runinga cha K24, Manduku alisema kwamba baada ya rais Ruto kupendekeza Kithure Kindiki kama naibu rais kufuatia kubanduliwa kwa Rigathi Gachagua, ODM wamemezea mate wadhifa ulioachwa wazi na Kindiki.
Alisema kwamba jina la Junet Mohammed limewasilishwa kwa rais Ruto kutathmini iwapo anaweza kuteua kama waziri wa ndani kumrithi Kindiki na baadae kuliwasilisha jina lake bungeni kupigwa msasa.
“Kindiki harudi tena katika wizara ya masuala ya ndani. Hiyo nafasi kwa sasa iko wazi. ODM tayari tumewasilisha jina la Junet Mohammed kwa rais. Sisi tumefanya tu kupendekeza, ni wajibu wa rais kufanya uamuzi,” Manduku alisema.
Mbunge huyo alifichua kwamba hata awali walikuwa wamependekeza jina la gavana wa Homabay Gladys Wanga kuteuliwa kama naibu rais baada ya Gachagua kubanduliwa.
Alisema hata hivyo rais alifikiria kivingine na kumchagua Kithure Kindiki, akisisitiza kwamba kwao wanapendekeza tu pengine rais anaweza ongeza ODM wadhifa mwingine katika serikali yake.
“Ni kama tu tulivyofanya kupendekeza jina la Gladys Wanga, lakini haikuzaa matunda. Na sasa tumependekeza jina la Junet, huenda ikazaa matunda au la. Uamuzi wa mwisho uko mikononi mwa rais,’ aliongeza.
Ikumbukwe ODM tayari wamevuna pakubwa kutoka kwa serikali jumuishi iliyozaliwa kutokana na shinikizo la maandamano ya vijana wa Gen Z.
Maandamano hayo yaliona rais Ruto akiwa chini ya shinikizo kiasi kwamba alifikia uamuzi wa kulivunja baraza lote la mawaziri.
Wiki moja baadae, alitangaza majina ya mawaziri wapya, wanne wakiwa kutoka chama cha ODM ambacho licha ya dalili zote kuonyesha wako ndani ya serikali, kinara wao Raila Odinga amekuwa akisisitiza bado ODM wako upinzani kama moja ya vyama vinavyounda muungano wa Azimio.
ODM tayari inajivunia mawaziri Oparanya, Joho, Mbadi na Wandayi katika serikali jumuishi
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!