Bifu la Marioo na aliyekuwa dancer wake, Chino Wanaman ambaye baadae alianza safari yake kama mwanamuziki wa Amapiano ya Uswahili linazidi kutokota baada ya wawili hao kuonekana kupapurana mitandaoni tena.
Hii ilianza upya baada ya Chino kuwashukuru watu kwa kutomtaja Marioo katika orodha ya watu waliomsaidia kupaa kimuziki, baada ya kushinda tuzo ya msanii bora kitengo cha machipukizi.
Marioo alielekea kwenye Instagram yake na kuachia ujumbe mrefu akitaka kujua ni nini hasa alichomfanyia vibaya Chino kiasi kwamba analazimisha bifu naye kwenye mitandao ya kijamii.
Marioo alieleza kwa uchungu jinsi amejitahidi mara kadhaa kukaa mbali na ugomvi na Chino lakini kinaya ni kwamba dogo huyo anajaribu kufanya kila kitu ili ionekane wao ni maadui.
“Ndugu zangu naomba mnisaidie kumuuliza Chino ni nini niliwahi kumkosea ambacho mimi sikijui zaidi ya kumuonyesha upendo na kumsupport.
Hili suala nimelikalia kimya muda mrefu sana lakini sasa naona imekuwa too much na mimi pia ni binadamu,” Marioo alieleza.
“Kila ninapojitahidi kutengeneza mazingira ya Amani na kukubali kuoneka na fala ili kila mtu aishi maisha yake, wananiona mimi mnyonge.
Hivi ni nani kamwambia Chino kuwa akitaka kuendelea kimuziki ni lazima anidharaulishe na aonekane ana matatizo na mimi?” Marioo alihoji zaidi.
Cha kushangaza, msanii huyo alikwenda hatua zaidi na kuibua madai kwamba anahisi wakati alikuwa amelazwa, Chino huenda ndiye alikuwa nyumba ya njama ya kumtilia sumu.
“Hii chuki imekuwa kubwa sana kiasi kwamba naanza kuamini kwamba pengine ni yeye alihusika kutuma watu waniwekee sumu ambayo nashukuru Mungu tulifanikiwa kuiwahi hapo siku zilizopita.
Kwa sababu pia yapo maneno tunayoyasikia akisema kwamba kitu kinachomsumbua ni mimi kutajwa kwenye historia ya maisha yake, kweli ndio tumefikia huku?” Marioo alisema akiambatanisha na picha akiwa amelazwa hospitalini.
Wawili hao wamekuwa katika uhusiano baridi kwa muda sasa baada ya Chino kujitoa katika kikosi cha wacheza densi ambao walikuwa wanafanya kazi chini ya Marioo.
Chino, ambaye alikuwa anamchezea densi Marioo aliondoka mapema mwaka jana na kuanza safari yake ya kuimba miziki ya Amapiano.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!