Wafungwa zaidi ya 100 walitoroka gerezani CHAD

Wafungwa zaidi ya 100 walitoroka kutoka gereza la usalama wa juu nchini Chad kufuatia tukio la ghasia lililosababisha vifo vya watu watatu na kumjeruhi gavana wa jimbo aliyekuwa akikagua gereza hilo.

Tukio hilo lilitokea Ijumaa usiku katika gereza lililoko umbali wa kilomita tano kutoka mji wa Mongo, katikati mwa nchi hiyo, baada ya wafungwa kuzua vurugu.

Kwa mujibu wa Hassan Souleymane Adam, Katibu Mkuu wa Mkoa wa Guera ambako Mongo unapatikana, “Karibu watu 100 wametoroka, watatu wamefariki na wengine watatu wamejeruhiwa.”

Chanzo kutoka Mongo ambacho hakikutaka kutajwa jina kiliiambia shirika la habari la AFP kwamba wafungwa walivamia ofisi ya msimamizi wa gereza na kupora silaha.

“Baada ya hapo, walikabiliana kwa risasi na walinzi, na hapo ndipo gavana alipowasili na kujeruhiwa,” alisema afisa huyo, akiongeza kuwa jumla ya wafungwa waliotoroka ni 132.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Afisa huyo alisema kuwa chanzo cha ghasia hizo ni malalamiko ya wafungwa kuhusu ukosefu wa chakula gerezani.

Waziri wa Sheria wa Chad, Youssouf Tom, alisema kwa njia ya simu kuwa alikuwa akielekea katika eneo la tukio na angeweza kutoa “taarifa sahihi mara tu atakapofika Mongo katika saa chache zijazo.”