
Maafisa wa usalama kutoka kikosi maalum cha mashirika mbalimbali mnamo siku ya Ijumaa walifanikiwa kumkamata mshukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya, Jane Njeri Muigai, mwenye umri wa miaka 28, akiwa na gramu 294 za dawa aina ya cocaine zilizokuwa zimefichwa katika sehemu zake za siri.
Mshukiwa alinaswa baada ya basi lililokuwa likielekea Nairobi kutoka Moyale kusimamishwa katika barabara kuu na maafisa hao, waliokuwa wakitekeleza oparesheni ya kuwasaka wauzaji wa dawa za kulevya wanaotumia njia ya Kaskazini kuingiza mihadarati jijini.
Kulingana na taarifa ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) iliyotolewa Aprili 18, tabia ya mshukiwa iliwatia wasiwasi maafisa wa kike waliokuwa kwenye doria, na kupelekea kumuweka kando kwa uchunguzi wa kina.
"Alionyesha hali ya wasiwasi isiyo ya kawaida, na kwa uzoefu wetu, hatia hujidhihirisha kwa tabia," DCI walisema katika taarifa.
Baada ya uchunguzi wa kina, maafisa waligundua dawa hizo aina ya cocaine zikiwa zimefichwa kwa njia ya ujanja katika mwili wa mshukiwa.
Mshukiwa amewekwa rumande katika Kituo cha Polisi cha Moyale huku maafisa wa Kitengo cha Kukabiliana na Dawa za Kulevya wakichukua jukumu la kuendeleza uchunguzi na kuanzisha hatua za kisheria dhidi yake.
“Tutahakikisha uchunguzi unakamilika haraka na ushahidi wote kuwasilishwa mahakamani ili mshukiwa afikishwe mbele ya sheria,” taarifa ya DCI ilisema zaidi.
Operesheni hii ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kupambana na ulanguzi wa dawa za kulevya, hasa katika maeneo ya mipakani ambayo yamekuwa njia kuu ya usafirishaji wa mihadarati.
DCI imesisitiza kuwa oparesheni kama hizi zitaendelea kote nchini, na kuwataka wananchi kushirikiana kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukomesha biashara hiyo haramu.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!