
Katika tukio la kushangaza lililozua msisimko mtandaoni, mwanamke mmoja kutoka eneo la Awasi, Kaunti ya Kisumu, amejikuta mikononi mwa sheria baada ya kupakia picha kwenye WhatsApp akionesha bastola aina ya Canik na kuambatanisha na tishio kwa wanaume wote waliodhamiria kumtema.
Kisa hiki kimegeuka kuwa cha kipekee kwa kuchanganya mapenzi, mitandao ya kijamii, na jinai ya kumiliki silaha isivyo halali.
Katika taarifa iliyotolewa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Jumanne jioni, Aprili 15, Sharon Auma alikamatwa na maafisa kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Uhalifu wa Kijasusi – Eneo la Nyanza kwa kushiriki vitendo vinavyohusiana na bunduki haramu na kutishia usalama kupitia mitandao ya kijamii.
Sharon anadaiwa kupakia picha kwenye WhatsApp status akionekana akishika bastola, huku ujumbe wake wa kutisha ukisomeka: “Mwanaume yeyote atakayeniacha ataona cha mtema kuni.”
Hii iliwachochea wapelelezi kuanza msako wa haraka uliozaa matunda.
Kwa mujibu wa DCI, alipokamatwa mjini Awasi, mshukiwa aliwaelekeza maafisa hadi kwa rafiki yake, Nancy Atieno, ambako walidai bunduki hiyo ilikuwa imefichwa.
Msako uliofanyika katika nyumba ya vyumba viwili ya Nancy ulizaa matokeo: bunduki hiyo ilipatikana ikiwa imefungwa kwa nguo ndani ya beseni chini ya kitanda, ikiwa na magazine tupu.
Aidha, wapelelezi walipata namba bandia ya usajili wa pikipiki: KMGG 805M.
“Tunachukulia suala hili kwa uzito mkubwa. Bunduki si chombo cha kutatua masuala ya mapenzi, na vitisho vya aina hii ni kosa la jinai,” alisema afisa mmoja wa DCI.
Wanawake hao wawili sasa wanazuiliwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani punde uchunguzi utakapotamatika, huku maafisa wakiendelea kuwinda washirika wengine wanaoweza kuhusika na silaha hiyo.
Kisa hiki kinazua maswali mapya kuhusu athari za mitandao ya kijamii na jinsi mapenzi yanavyoweza kuchukua mkondo hatari.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!