
Mbunge wa Homa Bay Town, Peter Kaluma, ametoa wito kwa mamlaka kuchukua hatua za haraka dhidi ya Mtume James Ng’ang’a wa Kanisa la Neno Evangelism Centre.
Hii ni kufuatia tukio lililonaswa kwenye video ambapo mhubiri huyo maarufu anaonekena akimpiga kofi muumini wakati wa ibada.
Katika video hiyo inayosambaa mitandaoni, Ng’ang’a anaonekana akimkaribia jamaa aliyeketi mstari wa mbele na kumshutumu kwa kulala wakati wa mahubiri.
Mhubiri huyo kisha anaonekana akimpiga kofi muumini huyo mara mbili kisha kumuamuru aketi nyuma ya kanisa.
“Amka! Nenda ukaketi kule nyuma,” Ng’ang’a anasikika akisema.
Punde baada ya hayo anamgeukia mwanamke aliyekuwa ameketi karibu na jamaa huyo na kumuuliza kwa sauti ya ukali, “Kwani huyu alikuwa analala na wewe unamtazama tu?”
Mwanamke huyo anajibu kuwa alikuwa amezingatia mahubiri na hakugundua kuwa jirani yake alikuwa amelala. Hata hivyo, Ng’ang’a anamwamuru pia kwenda kuketi nyuma.
Huku akijitetea, mwanamke huyo anasema: “Kila mtu abebe msalaba wake.”
Ng’ang’a anasikika akijibu, “Sawa, umewachiliwa,” kisha anarudi kwenye mimbari."
Mbunge Kaluma amelaani kitendo hicho, akiwataka wote waliowahi kupigwa au kushuhudia matukio kama hayo kutoka kwa mhubiri huyo waripoti mara moja katika kituo cha polisi kilicho karibu au wamtafute yeye moja kwa moja kwa hatua za haraka.
Aidha, ameiomba Ofisi ya Msajili wa Mashirika kuingilia kati suala hilo ili kuzuia madhara zaidi.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!