Waziri Aden Duale alikutana na wawakilishi wa KMPDU mnamo Aprili 10, 2025.

Muungano wa Madaktari, Wanadawa na Madaktari wa Meno wa Kenya (KMPDU) umetangaza mafanikio kadhaa muhimu kufuatia mkutano wake wa kwanza na Waziri mpya wa Afya, Aden Duale, uliofanyika Alhamisi, Aprili 10.

Mazungumzo hayo yaliangazia matatizo sugu katika sekta ya afya, ikiwemo ucheleweshaji wa ajira kwa madaktari waliohitimu wanaofanya mafunzo kwa vitendo, malimbikizo ya mishahara, ada za mafunzo ya uzamili, na changamoto za bima ya matibabu kwa wahudumu wa afya.

Kulingana na KMPDU, madaktari waliohitimu ambao wamekuwa wakingoja kupelekwa kazini wataanza kupiga kura ya mchujo mwezi huu, huku ajira zikipangwa kuanza tarehe mosi Julai 2025.

“Tumekubaliana kuwa ajira za madaktari waliohitimu zitaanza rasmi mwezi Julai. Hata hivyo, Waziri ameomba muda wa wiki tatu kuzungumza na Hazina Kuu, Baraza la Mawaziri na Rais kuhusu bajeti ya kuwalipa kulingana na makubaliano ya CBA,” alisema Katibu Mkuu wa KMPDU, Dkt. Davji Atellah.

Kuhusu malimbikizo ya mishahara, Dkt. Atellah alifichua kuwa wizara imekubali kulipa madaktari walio chini ya serikali kuu kufikia tarehe 31 Mei 2025, huku zoezi la kuthibitisha kiasi halisi la malipo likitarajiwa kuanza Jumanne, Aprili 15.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Zaidi ya madaktari 1,000 waliokuwa kwenye ajira za kaunti lakini hawakulipwa katika awamu ya Desemba/Januari watalipwa kufikia mwisho wa Aprili,” aliongeza.

“Awamu ya mwisho ya malipo inatarajiwa kati ya Julai na Agosti mwaka huu,” aliongeza.

Kwa upande wa bima ya afya, CS Duale aliahidi kuingilia kati kuhakikisha kuwa watumishi wa umma hawazuiliwi kutumia huduma za Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kwa sababu ya michango iliyochelewa.

“Tunatarajia suala hili litapatiwa suluhisho ndani ya wiki mbili,” alisema Dkt. Atellah.

Pia, madaktari 114 waliokuwa wakifanya kazi chini ya mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC) wakati wa janga la COVID-19, watahamishiwa ajira za kudumu zenye mafao ya pensheni ndani ya wiki tatu, baada ya mashauriano ya mwisho na Baraza la Magavana.

Katika hatua nyingine, Waziri Duale aliagiza Idara ya Afya ya Umma na Viwango vya Kitaaluma kuhakikisha kuwa madai ya ada za mafunzo kwa madaktari wa uzamili yanakaguliwa na kulipwa ndani ya siku 30.

Kuhusu marekebisho ya mishahara, Dkt. Atellah alisema:“Waziri amejitolea kushirikiana na Baraza la Magavana kuhakikisha kuwa mishahara mipya ya msingi imewekwa kwenye bajeti, na itaonekana kwenye pay slip kuanzia Julai au Agosti mwaka huu.”

Mkutano huo umechukuliwa kama hatua chanya ya kurejesha imani kati ya chama hicho na serikali.

“Hatua zilizofikiwa ni za kutia moyo, lakini kazi bado ipo mbele yetu. Tutafuatilia kwa karibu kuhakikisha kila ahadi imetekelezwa kikamilifu,” Dkt. Atellah alisema.”