Barack Obama and Michelle Obama

Michelle Obama hatimaye amezungumzia uvumi ulioenea kuhusu matatizo kwenye ndoa yake na rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama.

Kutokuwepo kwake katika hafla muhimu kama vile kuapishwa kwa Donald Trump na mazishi ya rais wa zamani Jimmy Carter kumeibua tetesi kuwa huenda wawili hao walikuwa wakitengana.

Hata hivyo, kupitia mahojiano katika podikasti ya Work in Progress inayongozwa na mwigizaji Sophia Bush, Bi Obama alifafanua mambo, japo hakuzitaja hafla hizo moja kwa moja. Alisema kuwa akiwa mwanamke mzima sasa, anaweza kupanga ratiba yake mwenyewe.

“Kuna watu hawaamini kuwa ninaweza kufanya maamuzi yangu binafsi,” alieleza. Badala yake, walihisi kuwa mimi na mume wangu tunatalakiana.”

Bi Obama alikiri kuwa kujiondoa kwenye baadhi ya majukumu kulimletea hisia za hatia, jambo analoamini kuwa linawakumba wanawake wengi.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Hilo ndilo jambo ambalo wanawake tunapambana nalo—hofu ya kuwaangusha watu,” alisema.

Aliongeza, “Mwaka huu watu walishindwa kabisa kuamini kuwa nilikuwa nafanya maamuzi yangu. Ilibidi waamini tunatalakiana. Hii haiwezi kuwa mwanamke mzima anayefanya maamuzi kwa ajili yake mwenyewe, sivyo? Lakini ndivyo jamii inavyotutendea.

Akiendelea kufafanua, alieleza: “Nilichagua kufanya kilicho bora kwangu. Sio kilichonilazimu, wala kile nilichodhani watu walitaka nifanye.”

Licha ya kutohudhuria hafla kadhaa za kimila, Michelle Obama bado yumo kwenye shughuli za umma. Majira ya kiangazi yaliyopita, alihutubia kwa kishindo katika Kongamano la Kitaifa la Democratic (DNC), akimnadi Kamala Harris huku akisema mbele ya umati jijini Chicago, “Tumaini linarejea.”

Alibainisha pia kuwa licha ya kutumia muda zaidi kwake binafsi, bado anashiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii. “Bado ninatoa hotuba, nipo duniani nikifanya kazi mbalimbali, na bado ninajali elimu ya wasichana.”

Mwezi Oktoba mwaka jana, familia ya Obama iliadhimisha miaka 32 ya ndoa.

Katika kitabu chake maarufu Becoming, Bi Obama alielezea kwa uwazi changamoto walizokumbana nazo kwenye ndoa yao, hasa kutokana na ndoto za kisiasa za mumewe ambazo mara nyingi zilimuacha akiwa mpweke na mchovu.