Jumba hatari ambalo lilibomolewa Mombasa likiporomoka 

Baada ya saa nne na nusu za kupanga kwa uangalifu, maafisa wa Jeshi (KDF) Jumatano alasiri walifanikiwa kubomoa jengo hatari la orofa 11 lililokuwa limelegea wakitumia vilipuzi vilivyodhibitiwa.

Jengo hilo lililo katika eneo la Kilifi katika Kaunti Ndogo ya Mvita, lilikuwa limeonyesha dalili za kuanguka baada ya kuanza kuzama kutokana na kasoro kubwa za kimuundo na msingi.

Sehemu ya jengo tayari ilikuwa imezama baada ya kisima kuchimbwa karibu na msingi wake bila idhini.

Siku ya Jumanne alasiri, serikali ya kitaifa na ile ya kaunti zilitangaza kuwa KDF itatekeleza ubomoaji huo kwa kutumia vilipuzi - uamuzi ambao ulizua wasiwasi miongoni mwa wakazi, ambao wengi wao waliiona operesheni hiyo kuwa hatari.

Awali gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir alikuwa ameeleza kuwa shughuli hiyo ingechukua takriban saa nane kukamilika.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Wakazi wote wanaoishi ndani ya eneo la kilomita 1.2 waliamriwa kuondoka katika nyumba zao, huku biashara, shule na hospitali katika eneo hilo pia zikifungwa kwa usalama.

Daraja la Nyali, linalounganisha Kisiwa cha Mombasa na Pwani ya Kaskazini, lilifungwa kuanzia saa 7:30 asubuhi pande zote mbili.

Mwendo wa saa saba unusu alasiri polisi pia walifunga barabara ya Fidel Odinga huko Nyali.

Mlipuko mmoja wenye nguvu ulisikika takriban saa saba 55 alasiri na baada ya sekunde chache, jengo hilo lilibomoka - operesheni iliyoonyesha usahihi wa KDF na utaalam wa kijeshi.

Hapo awali mlipuko huo ulikuwa umecheleweshwa baada ya mamlaka kusema kuwa baadhi ya wakazi walikuwa bado hawajaondoka eneo hilo. Eneo hilo lilikuwa na takriban wakaazi elfu 60.

Zaidi ya wagonjwa 289 waliokuwa wamelazwa katika Hospitali Kuu ya Mafunzo na Rufaa ya Pwani pia walihamishiwa katika vituo vingine vya afya vya kaunti nje ya eneo la Mvita.

Soko la Marikiti lenye shughuli nyingi pia lilifungwa, bila biashara kuruhusiwa, kwani liko ndani ya eneo lililozuiliwa la kilomita 1.2.