
Bi Dottie Nzilani, mzazi mwenza wa marehemu mwanahabari Nick Mudimba, anaendelea kuomboleza kifo chake kilichotokea ghafla mwezi uliopita.
Nick alipoteza maisha mnamo Machi 23 baada ya kuanguka ghafla, na alizikwa siku ya Jumamosi, Aprili 5, katika eneo la Gem, Kaunti ya Siaya.
Familia, marafiki, wenzake kazini, majirani na mashabiki walijitokeza kwa mamia kumuaga mwanahabari huyo aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 37. Dottie, ambaye ana binti wa miaka tisa na marehemu, pia alihudhuria mazishi hayo.
"Jina langu ni Dottie. Nick alikuwa baba mzuri na aliyekuwa karibu sana na binti yetu. Tumesikitika sana kumpoteza, hasa mwanangu. Asanteni," alisema Dottie wakati wa mazishi.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumatatu, mama huyo wa binti mmoja alielezea ugumu wa kukabiliana na kifo cha Mudimba.
Dottie alibainisha kuwa binti yao wa miaka tisa ameathirika sana na msiba huo, na akatoa shukrani kwa wote waliowaunga mkono katika kipindi hiki kigumu.
“Wiki mbili zilizopita zimekuwa ngumu sana kwetu, hasa kwa mwanangu. Katika umri wake mdogo, amepitia pigo kubwa sana. Nataka kuwashukuru kwa maneno yenu ya faraja, maombi na msaada wenu. Familia, marafiki na hata watu nisiowajua wamejitokeza kutuunga mkono. Asanteni!” aliandika kupitia Instagram.
Dottie aliambatanisha ujumbe wake na picha kadhaa zinazoonesha kumbukumbu nzuri kati ya marehemu na binti yao.
Alizungumzia pia huzuni waliyo nayo na kueleza kuwa kifo cha Mudimba kimeacha pengo kubwa katika maisha yao.
“Nick, huenda hatuelewi mapenzi ya Mungu, lakini tunachoweza kusema ni pumzika salama. Tunasikitika, tunaumia sana, tumechanganyikiwa. Umeacha pengo kubwa sana kwenye maisha yetu ? Tutakukosa mno. Tutakupenda milele ??? PUMZIKA SALAMA ?️?️?️,” alisema.
Marehemu Mudimba ameacha mjane wake, Winnie Chege, binti yao wa miaka tisa Shanice Minoo, na mtoto mwingine ambaye bado hajazaliwa.
Mjane huyo, ambaye anatarajiwa kujifungua mwezi huu, pia alitoa ujumbe wa majonzi, akikumbuka nyakati nzuri walizoshiriki pamoja.
Mudimba alianguka na kufariki dunia alipokuwa akitazama mechi kati ya Kenya na Gabon katika makazi yake eneo la Syokimau mnamo Jumamosi, Machi 23.
Mwanahabari huyo aliyefariki akiwa na miaka 37 alikuwa amegunduliwa kuwa na kiwango cha juu cha asidi ya uric, na alipewa dawa siku ya Jumapili, saa chache kabla ya kifo chake.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!