Nuru Okanga, Oscar Sudi

NURU Okanga ametoa wito kwa mbunge wa Kapseret Oscar Sudi kumalizia kumlipa deni la ahadi aliyompa mwaka jana.

Wawili hao walikutana kwenye Obinna Show ambapo Sudi aliahidi kumpa Okanga shilingi milioni 1.3 kwa ajili ya kufungua biashara.

Akizungumza katika mazungumzo na kituo kimoja cha redio humu nchini siku chache zilizopita, Okanga alikiri kwamba Sudi alitimiza ahadi hiyo japo kwa nusu.

Okanga alilaumu vyombo vya habari kwa kuchangia kutopewa ahadi yote ya Sh1.3 na kupewa Sh700k pekee, kwani Sudi aligoma kumalizia deni hilo baada ya Okanga kulizungumzia kwa wanahabari.

“Oscar Sudi alinipa Sh700k taslimu na mimi namheshimu. Lakini unajua watu wa media ndio walizua cheche wakati waliniuliza kuhusu salio. Nikijibu inaonekana ni makosa. Salio sikupewa, na huo ndio ukweli wa mambo,” Nuru Okanga alisema.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Hata hivyo, alimtaka Sudi kutii ahadi yake ya kumalizia salio lililobaki kutoka kwa Sh1.3m kwani ahadi hiyo aliiweka hadharani na kila mtu akasikia na kuona.

“Nilipewa Sh700k na niliridhika, lakini maelewano yalikuwa Sh1.3m, na kwa sababu uliweka makubaliano mbele ya Wakenya, mbona usitimize?” Okanga alimwambia Sudi.

Hata hivyo, kando na kulaumu wanahabari kwa kile alidai ni kuchonganisha uhusiano wake na Sudi, pia alisema kuwa huenda yeye mwenyewe ni wa kulaumiwa kutokana na cheche zake dhidi ya serikali.

Okanga alisema kwamba Sudi alivuta nyuma kidogo kumalizia Sh600k zenye zilikuwa zimebaki kutoka kwa ahadi hiyo baada ya kuona kwamba anaishambulia serikali.

Ikumbukwe Oscar Sudi ni mwandani na mtetezi mkali wa serikali ya rais William Ruto ambayo Nuru Okanga amekuwa akiishambulia na kuikosoa bila kusita.

“Salio lilikuwa limebaki Sh600k na hayo maneno wakati aliona nimedinda kuunga serikali mkono, ni kama aliruka makubaliano,” Okanga alisema.

Kuhusu alichofanyia Sh700k alizopokea, Okanga alisema zilimsaidia kwa njia kubwa kwani aliweka mradi mkubwa wa kujikimu kibiashara nyumbani kwao, Kakamega.

“Nilienda nyumbani nikafanya vitu vingi, nilinunua poshomill, nikalipia watoto wengine karo ya shule, nikaweka mradi wa ufugaji wa kuku, nikakodisha shamba kidogo kidogo nimepanda mahindi, na miwa…” alieleza.