
GAVANA wa Nyeri, Mutahi Kahiga amekariri msimamo wake wa kusimama nan aibu wa rais aliyebanduliwa Rigathi Gachagua licha ya kuonekana kumkaribisha rais Ruto katika ngome hiyo ya Mlima Kenya.
Akizungumza Alhamisi, Kahiga alijibu swali la wengi kuhusu kulegeza msimamo wake na kumkaribisha rais ambaye amekuwa akihasimiana na Gachagua tangu kubanduliwa kwake Oktoba mwaka jana.
Kwa mujibu wa Kahiga, kumkaribisha rais Ruto hakubabidi kwa njia yoyote msimamo wake na wa watu wa Mlima Kenya kwamba Gachagua ndiye mbabe wao wa kisiasa.
Gavana huyo wa Nyeri – kaunti ya nyumbani ya Gachagua – alifichua kwamba yeye na wengine kujitokeza kumkaribisha Ruto kwa mbwembwe ilikuwa tu kwa sababu ya zawadi alizopelekea eneo hilo.
“Si mimi mwenyewe nilimkaribisha Nyeri, mimi ni gavana na yeye ni rais na nilimpokea. Lakini hata yeye mwenyewe anajua uchangamfu uliokuwa mwanzo na ule uliokuwa wakati huu kuna tofauti kwa sababu kuna yale mambo ambayo yalitendeka ambayo hayajakuwa sawa kwa watu wa eneo hili.”
“Unajua watu wa Mlima Kenya huwa si watu wa kcuhangamka na kupiga nduru, wakikasirika huwa wananyamaza. Sasa juzi ndio maana ulisikia tulielezwa kwamba rais anakuja, tukaambiwa kwamba anatuletea zawadi, basi tukajitokeza na tumepata,” aliongeza.
Alimtumia rais ujumbe akimwambia kwamba eneo la Mlima Kenya bado lina mwenyewe na wala asijidanganye kufikiria kwamba makaribisho aliyopewa na watu wa eneo hilo ni ishara ya kutikisa ngome ya kisiasa ya Gachagua.
“Nataka niseme hivi, rais ni kingpin wa Kenya, lakini si kingpin wa Mlima Kenya. Ukimuona mwambie Mlima una wenyewe,” Kahiga alikariri.
Ruto amekuwa akizuru Maeneo mbalimbali ya eneo pana ya Mlima Kenya katika ziara yake ya kimaendeleo itakayokamilika wikendi hii.
Alianza ziara yake katika kaunti ya Laikipia na Nyeri ambako alipokelewa kwa mbwembwe na furaha na umati wa wakazi wa Maeneo hayo.
Mapokezi hayo yalizua tumbojoto miongoni mwa wandani wa Rigathi Gachagua ambaye awali aliwasisitizia watu akiwataka kususia ujio wa rais kwa kile alikuwa anasema kwamba alikuwa anawapelekea injili ya uongo na ahadi hewa.