
KATIKA kile ambacho wengi wanaweza kukiona kama adimu, kiongozi wa WIPER, Kalonzo Musyoka amefungua milango ya watu kupata uelewa wa Imani na misimamo yake ya kidini, mbali na siasa.
Katika simulizi ya kipekee kwenye TV47, Musyoka alifichua kwamba yeye huwa hapendi kunadi na kuzungumzia sana Imani yake na misimamo yake ya kidini lakini ukweli ni kwamba ana msingi dhabiti sana katika Yesu Kristo.
Kalonzo alisema wakati akiwa mwanafunzi chuoni, aliwahi kuwa kiongozi wa muungano wa kidini na mara nyingi hupenda sana kuimba.
“Wito wangu ni kwa kuwatumikia watu katika uongozi na hili nilianza kitambo sana nikiwa shule ya upili wakati nilikuwa naongoza muungano wa wanafunzi wakristo (CU) na hata chuoni wakati nilikuwa naongoza nyimbo za ibada katika kanisa la St Andrew’s.”
“Na kwa kweli huwa sipendi sana kuzungumza kuhusu Imani yangu, lakini hiyo ndiyo huniongoza na hicho ndicho ambacho kimenitengeneza. Watu wanaweza chukua kila kitu lakini sio Imani yangu katika Yesu Kristo,” Musyoka alieleza.
Kuhusu nyimbo ambazo anazipenda, Kalonzo alifichua kwamba anapenda sana kumsikiliza mwinjilasti kutoka Rwanda, Israel Mbonyi.
Alifichua kwamba wakati msanii huyo alizuru Kenya mwaka jana, alimualika nyumbani kwake ambapo alimuimbia na kumchezea gitaa mkewe, Pauline, ambaye amekuwa akiugua.
“Nilikuwa nasikiliza tungo za Israel Mbonyi, kijana huyo kwa kweli alikuja na akamchezea mke wangu gitaa. Kwa sababu watu wanajua kwamba Pauline amekuwa mgonjwa [kwa muda sasa] na hivyo Israel Mbonyi alikuja,” Kalonzo alifafanua.
Alifichua kwamba familia yake imebarikiwa sana na vipaji vya uimbaji, akigusia kwamba hata mke wake mwenyewe ni msanii wa injili.
“Mke wangu mwenyewe ni msanii wa injili na nafikiri hilo liko katika familia. Mwanetu ni mtunzi mzuri sana na hivyo ninapenda sana kuimba, hata miziki ya country,” alisema huku akipiga kionjo cha wimbo Nina Siri wake Israel Mbonyi.
Kalonzo pia aliwafichulia wakenya japo kwa kiduchu kuhusu jinsi anavyojiweka kimaisha kiasi kwamba anaonekana mdogo kuliko umri wake wa miaka 71.
Kulingana naye, hajawahi tumia pombe wala sigara katika maisha yake japo amekuwa akizungukwa na marafiki wanaotumia vilevi hivyo.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!