
Kocha wa Fenerbahce, Jose Mourinho, alizua tafrani kubwa baada ya kushindwa na Galatasaray kwa mabao 2-1 katika robo fainali ya Kombe la Uturuki mnamo Aprili 2, 2025.
Katika tukio lililoshangaza wengi, Mourinho alimkaribia kocha wa Galatasaray, Okan Buruk, na kumpinya puani, jambo lililozua ugomvi mkubwa kati ya benchi la ufundi na wachezaji wa pande zote mbili.
Galatasaray walipata ushindi huo kutokana na mabao mawili ya Victor Osimhen, huku Sebastian Szymanski akiifungia Fenerbahce bao la kufutia machozi.
Mchezo huo ulikuwa wa kasi na ushindani mkali, lakini mzozo ulizidi kuwa mkubwa wakati wa dakika za majeruhi, ambapo wachezaji watatu waliokuwa benchi walionyeshwa kadi nyekundu baada ya kushiriki katika ugomvi uliotokea uwanjani.
Baada ya filimbi ya mwisho, Mourinho alimfuata Buruk na kumfinya puani Baruk, hali iliyomfanya meneja huyo wa Galatasary kuanguka chini kwa mbwembwe.
Tukio hilo lilisababisha vurugu kubwa, huku maafisa wa usalama wakilazimika kuingilia kati ili kutuliza hali ya mambo.
Kitendo cha Mourinho kimeibua mjadala mkubwa, huku wakosoaji wake wakisema kuwa ni mwendelezo wa matukio yake ya utovu wa nidhamu katika historia yake ya ukocha.
Hii si mara ya kwanza kwa Mourinho kuhusika katika matukio ya aina hii. Mwaka 2011, alipokuwa kocha wa Real Madrid, alifungiwa kwa kumpiga kidole jichoni Tito Vilanova, aliyekuwa msaidizi wa kocha wa Barcelona wakati huo.
Mapema mwaka huu, alisimamishwa mechi kadhaa kwa kutoa matamshi ya kuwadhalilisha waamuzi wa ligi ya Uturuki.
Baada ya mchezo huo, klabu ya Galatasaray ilimkejeli Mourinho kwa kupakia picha yake na Buruk kwenye mitandao ya kijamii na kuweka ujumbe: "Hupaswi kushambulia, unapaswa kumeng'enya."
Hili limechukuliwa kama kejeli kwa Mourinho ambaye amekuwa akitoa matamshi ya kichokozi kwa wapinzani wake.
Kwa sasa, Fenerbahce wako nyuma kwa alama sita dhidi ya Galatasaray kwenye msimamo wa ligi, huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
Bado haijajulikana iwapo Shirikisho la Soka la Uturuki litachukua hatua dhidi ya Mourinho kutokana na tukio hilo, lakini wachambuzi wa soka wanaamini anaweza kuadhibiwa kwa tabia yake isiyo ya kiungwana.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!