Rachel Otuoma

TIKTOKER Rachel Otuoma amefunguka jinsi penzi lake na marehemu mwanasoka Ezekiel Otuoma bado lingalipo licha ya kumzika mwanasoka huyo takribani miezi 3 iliyopita.

Akizungumza kwenye shoo ya Oga Obinna, Rachel Otuoma alisema kwamba ahadi na kiapo chake cha kutoivua pete yao ya ndoa bado ingalipo, kwani hiyo ndio humpa ukumbusho wa kila kitu kizuri Otuoma alimfanyia enzi za uhai wake.

Pia alikariri kwamba hatoweza badili jina kwa kufuta lile la Otuoma katika utambulisho wake, akisema kuwa jina hilo limejinafasi katika sehemu ya upekee kwenye moyo wake.

“Jina Rachel Otuoma halitawahi badilika. Litakuwa jina langu la matumizi kwa muda wote wa maisha yangu. Otuoma mwenyewe alinipa jina hilo na mpaka anakufa, sikuwa mtalaka. Hakuna mahali popote niliandika kwamba mimi ni mtalaka, sema tu kifo ndicho kilitutenganisha hivyo sioni sababu ya kufuta jina lake,” Otuoma Rachel alijieleza.

Kuhusu kusonga mbele na maisha na kutafuta mpenzi mwingine, Rachel aliweka wazi kwamba ingawa uwezekano wa kupenda tena upo, lakini hafikirii kuingia katika uhusiano serious.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Alisema kwamba huenda akalazimika kuchagua mahusiano ya muda tu lakini suala la kuingia katika uhusiano wa kudumu ni kibarua kigumu kuushawishi moyo wake.

“Sidhani kama nitakuwa katika uhusiano wa kudumu tena, ni mahusiano wazi tu kwa sababu mwanamume wangu [Otuoma] atasalia daima katika moyo wangu na hii pete yake sitawahi ivua maana italeta shida,” Rachel alifafanua.

Pia alisimama kidete na kutetea uamuzi wake wa kuhama katika nyumba ambayo alikuwa akiishi pamoja na marehemu mume wake.

Kulingana naye, asingeweza kustahimili kuendelea kuishi katika nyumba ile kwa kile akitaja kuwa ilikuwa imejawa na kumbukumbu nyingi za nyakati zao pamoja hivyo hangeweza kupona kutokana na kifo cha mumewe.

Aliondoka ili kuzikwepa baadhi ya kumbukumbu hizo ambazo zingechelewesha safari yake ya kupona na kukubali kwamba Otuoma hatokuwepo maishani naye tena.

“Kulikuwa na kumbukumbu nyingi katika ile nyumba, hivyo nilifanya uamuzi wa kuhama ili nianze tena upya,” Rachel alisema.

Otuoma alifariki mwaka jana siku chache kuelekea Krismasi na kuzikwa Mapema januari baada ya kupambana na ugonjwa uliopooza neva zake za mwili kwa takribani miaka mitano.