
SEHEMU ya wachungaji katika kaunti ya Meru wamesema hawawezi kata michango ya pesa kutoka kwa wanasiasa huku rais Ruto akitarajiwa kutembelea kaunti hiyo katika ziara yake ya wiki moja eneo la Mlima Kenya.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika kaunti hiyo, wachungaji hao walisema kuwa hawawezi kataa pesa kwani hakuna pesa chafu wala ya dhambi.
“Kuna pesa tunaona zikipatiwa makanisa, unapata maaskofu wa kanisa kubwa kubwa wanasema pesa irudishwe. Sasa tunashangaa kama mimi hata kama naheshimu mafuta naheshimu kina baba wa kanisa, ningependa kuuliza kwa unyenyekevu, kuna ile njia inaweza tumika zinaweza saidia watu kwa sababu pesa si eti ni ya dhambi, hakuna pesa ya dhambi,” Alisema pasta Jediel Kirema.
Mchungaji huyo alisisitiza kwamba wachungaji wanahitaji pesa hizo kujikimu kimaisha ili kuweza kueneza injili kwa mwenendo unaofaa.
“Yale makanisa ambayo yanarudisha pesa mle ndani kuna makahaba, kwa kuwa hujui nia ya mtu, kuna wezi… na wote wanatoa pesa. Kwa hivyo pesa ni ya benki kuu ya Kenya, pesa haina shida, iletwe kwa njia za utaratibu.”
“Ziletwe ili zisaidie wachungaji wengine waache kutumia njia za ujanja kutafuta pesa, wakipata pesa za kujimudu kibiashara hata kazi ya Mungu itafanyika kwa njia halali, kwa hivyo hakuna pesa mbaya, rais pesa si mbaya, imetengenezwa na ni ya Mungu,” Kirema aliongeza.
Askofu James Gichuru pia aliradidi maneno hayo akisema kwamba rais Ruto amekaribishwa kutoa sadaka katika makanisa yao na kuahidi kwamba wao hawatarudisha sadaka.
“Tunajua na tumesikia kwamba mheshimiwa rais Ruto anakuja Meru. Sisi wachungaji tunamkaribisha Meru na tunamuomba pia akija asapoti sacco za wachungaji. Pesa kama zile zinapeanwa tukipewa sisi kama sacco zitasaidia wanachama wetu na tutaweza kujimudu, hatutakuwa watu wa kuomba omba, tutakuwa watu wa kujisimamia na kufanya mambo,” askofu huyo alisema.
Askofu huyo alibainisha kwamba wao hawako katika siasa bali wanaunga mkono uongozi wa serikali iliyopo kutoka kwa ngazi za kaunti hadi kitaifa.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!