Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga amethibitisha atawania urais 2027

Aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga, amethibitisha nia yake ya kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2027, akisema yuko tayari kuongoza mabadiliko ambayo taifa linahitaji.

Akizungumza baada ya ibada ya kanisa katika Kaunti ya Kisii Jumapili, Maraga alieleza kuwa ingawa ana azma ya kuwania kiti hicho, hatma yake iko mikononi mwa wapigakura.

Aidha, alikanusha vikali madai kwamba yeye ni mgombea anayependekezwa na watu fulani kwa maslahi yao binafsi.

"Hatimaye, wananchi ndio watakaoamua. Acheni wasiwasi, subiri na kwa wakati ufaao, mtajua iwapo mimi ni mgombea wa serikali au la," alisema Maraga.

Alitoa wito kwa Kamati ya Uteuzi ya IEBC kuhakikisha kuwa makamishna wapya watakaoteuliwa ni waaminifu na wenye uwezo wa kusimamia uchaguzi kwa haki na uwazi.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

"Tunaomba kwamba wale wanaochaguliwa wawe watu waadilifu, wenye nia ya kuhakikishia Wakenya uchaguzi huru na wa haki," alisisitiza.

Kauli yake inakuja wakati ambapo baadhi ya viongozi wa Kisii, wakiongozwa na Seneta Richard Onyonka, wanapendekeza aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i, kama mgombea wa urais wa jamii hiyo katika uchaguzi wa 2027.

"Tumeamua kama jamii kuwa tutaanzisha chama chetu cha kisiasa. Tutatoa mgombea wetu ambaye atazungumza na Rais na viongozi wengine wa kisiasa, na huyo si mwingine bali ni Fred Matiang’i," alisema Onyonka.

Hivi majuzi, Maraga alikubali idhinisho kutoka kwa kizazi cha Gen Z kuwania urais, akisema kuwa anashauriana na wadau mbalimbali kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

Akihutubia wanafunzi na wanajamii katika Chuo Kikuu cha Rongo mnamo Machi 27, Maraga alisema ataweka wazi msimamo wake rasmi pindi atakapokamilisha mashauriano.

"Nimepokea ombi hilo na ninalijadili na wadau tofauti. Nitatangaza uamuzi wangu wa mwisho, na wakati ukifika, tutajua iwapo nitawania au la," alisema.

Maraga alisisitiza kuwa yeyote anayewania wadhifa wa kuchaguliwa lazima awe na dhamira ya kuwahudumia wananchi kwa mujibu wa matakwa ya ofisi hiyo.

Alionyesha utayari wake wa kuongoza taifa, akirejelea uzoefu wake alipohudumu kama Jaji Mkuu. "Niliongoza mhimili mmoja wa serikali, na hakuna miujiza katika kuongoza mhimili mwingine," alisema.

Akizungumzia changamoto kubwa zinazolikabili taifa, Maraga alitaja ufisadi kama kikwazo kikubwa kwa maendeleo nchini.

"Tatizo kuu nchini ni rushwa. Kuna ufisadi wa bajeti na wa kitaasisi ambao haujashughulikiwa ipasavyo. Matokeo yake ni kwamba taifa halina rasilimali za kutosha kushughulikia changamoto zilizopo," alisema Maraga.