Beatrice Elachi akizungumza wakati wa mazishi ya mwanawe

Mbunge wa Dagoretti North, Beatrice Elachi, ambaye bado anaomboleza, amefichua kuwa marehemu mwanawe, Elvis Murakana Namenya, alikuwa kijana mwenye afya njema kila wakati.

Akizungumza siku ya Jumamosi katika ibada ya mazishi kabla ya kumpumzisha kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 katika kijiji cha Nalepo, Kaunti ya Kajiado, Elachi alieleza kuwa mwanawe hakuwahi kulazwa hospitalini kabla ya ajali mbaya iliyosababisha kifo chake.

Elachi alimshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya mwanawe na kuenzi miaka aliyopata kuishi.

"Leo ni siku ya kusema asante kwa Mungu. Pia nawashukuru nyote maana sijui nianzie wapi wala niseme nini," alisema kwa waombolezaji waliokusanyika Jumamosi kumuaga mwanawe.

"Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu maana ndiye aliyenipa huyu kijana. Alikuwa kijana ambaye hajawahi kuenda hospitali. Hii ilikuwa mara yake ya kwanza na ya mwisho. Tunasema Amina," aliongeza.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Elvis, aliyefariki Machi 25, 2025, baada ya wiki moja katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), hatimaye alipumzishwa katika makazi ya wazazi wake katika kijiji cha Nalepo, Kaunti ya Kajiado. Hali ya hewa ya mvua ilitanda siku hiyo, huku familia, marafiki, wanasiasa, na wakazi wa eneo hilo wakikusanyika kutoa heshima zao za mwisho kwa kijana huyo.

Akizungumza katika ibada ya kumbukumbu iliyofanyika katika Kanisa la Holy Trinity, Kileleshwa, Ijumaa, Machi 27, Elachi alieleza kwa kina namna ajali iliyochukua maisha ya mwanawe ilivyotokea, akifichua kuwa Elvis alipata jeraha kubwa kichwani lililosababisha ubongo wake kuathirika vibaya.

Kwa mujibu wa Elachi, Elvis alikuwa akirejea nyumbani baada ya kukutana na rafiki yake alipokumbwa na tatizo la gurudumu kutoboka ghafla. Kwa kushindwa kuidhibiti hali hiyo, gari lake liligonga vibaya, na majeraha aliyoyapata yakapelekea kifo chake.

“Nataka kuzungumza na wazazi kuhusu watoto wetu leo. Tuna kizazi kinachoamini kuwa kinaweza kushughulikia changamoto zao peke yao. Wanaweza kuamka muda wowote kusaidiana bila hata kutufahamisha. Watatuambia tu ikiwa hawawezi tena kusuluhisha hali hiyo. Lakini wanasaidiana sana, na mara nyingine hata hatujui kinachoendelea,” alisema.

Mbunge huyo alitumia fursa hiyo kuzungumzia usalama barabarani, hasa jinsi ya kushughulikia pancha wakati wa kuendesha gari.

“Elvis alikuwa tayari amelala saa nne na nusu usiku alipigiwa simu kuhusu kazi fulani. Alienda haraka na kuimaliza. Lakini alipokuwa akirejea, gari lake likapata pancha. Vijana wengi hawajui kuwa gari likipata pancha, hupaswi kabisa kubana breki za dharura. Gari litatereza, na hapo ndipo unaweza kupoteza mwelekeo kabisa. Unachopaswa kufanya ni kushikilia usukani kwa nguvu, kuhakikisha gari linapunguza mwendo polepole, na kumwomba Mungu lisimame salama. Kwa bahati mbaya, Elvis alipata jeraha baya sana—ubongo wake ulitoka mahali pake, na hilo ndilo lililosababisha kifo chake,” alieleza.

Elachi alisimulia pia jinsi alivyomtazama mwanaye akiwa ICU siku ya Jumamosi na kufahamu kuwa hangeweza kupona.

"Sikuambia hata madaktari, lakini nilipomtazama, nilijua tu—anaenda zake," alisema kwa huzuni.

Akimzungumzia marehemu mwanaye, mbunge huyo alisema Elvis alikuwa kijana aliyependa sana kanisa, muziki, na soka. Ingawa alikuwa mtu wa kujitenga, alipenda sana mpira wa miguu, na kadri alivyokua, alipata mapenzi makubwa kwa muziki

"Lakini jambo moja nitawaambia, alipenda sana kanisa hili. Na hata ninapokuja hapa, ukiwauliza watu wa Holy Trinity, sijawahi kuja kama 'Mheshimiwa'," aliongeza.

Elachi alihitimisha kwa kumwomba Mungu amrehemu na kumfungulia Elvis mlango wa mbinguni, ili apate pumziko la milele.