
WAZIRI wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen ametembea nyumbani kwa mbunge wa Dagoretti Kaskazini Beatrice Elachi kuifariji familia yake kufuatia kifo cha mwana wao, Elvis Murakana.
Waziri huyo alichapisha picha kwenye ukurasa wake wa X akimfariji mbunge Elachi kwa kumpa kumbato la faraja kufuatia pigo hilo.
“Jioni ya leo nilimpa pole dada yangu Mhe. Beatrice Elachi kufuatia msiba wa kufiwa na mwanawe Elvis Murakana. Mungu amjalie neema na familia yake katika kipindi hiki kigumu cha msiba,” Murkomen aliandika kwenye chapisho lake.
Elvis Murakana Namenya alifariki kufuatia ajali ya barabarani mnamo Machi 25, 2025.
Alikuwa mwanafunzi wa Masomo ya Biashara katika Chuo Kikuu cha Africa Nazarene na alikuwa akisubiri kwa hamu kuhitimu mnamo Juni mwaka huu.
Kwa mujibu wa familia, shughuli za kumuaga rasmi zitaanza Alhamisi, Machi 28, 2025, kwa ibada ya wafu itakayofanyika katika Kanisa la Holy Trinity, Kileleshwa, kuanzia saa nne asubuhi.
Familia imesema kwamba Elvis, mwenye umri wa miaka 26, alikuwa kijana mwenye ndoto kubwa, na kifo chake kimeacha simanzi kubwa kwa familia na marafiki.
Viongozi wengine walioifariji familia ya Elachi ni pamoja na rais Ruto.
“Mungu amtie nguvu Mheshimiwa Beatrice Elachi na familia nzima kuhimili msiba wa mtoto wao mpendwa, Elvis Murakana. Ufarijiwe na neno la Bwana katika Zaburi 147:3: “Huwaponya waliovunjika moyo, na kuzifunga jeraha zao.” Pumzika kwa Amani Elvis,” Ruto aliandika.
Elvis alizaliwa Septemba 13, 1998, na atapumzishwa Machi 29, 2025.
Marehemu alikaa kwa wiki moja katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya AAR baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani mapema wiki jana.
Inasemekana kuwa aliondoka nyumbani kuelekea Kasarani kwa shughuli zake mnamo Jumanne, Machi 18, ambapo ajali hiyo ilitokea.
Kwa bahati mbaya, alipokuwa akirejea nyumbani, gari lake lilipasuka gurudumu akiwa barabara ya Thika, na kusababisha likengeuke na kugonga uzio wa usalama.
Polisi walipofika eneo la tukio, walimkuta Elvis akiwa amepoteza fahamu na wakamkimbiza mara moja katika Hospitali ya AAR kwa matibabu ya dharura.