Akili mnemba (AI)

WANAFUNZI wa utandawazi katika chuo kikuu cha Zetech wamefanikiwa kuunda programu ya akili mnemba (AI) ambayo imetajwa kuwa itakayoleta mabadiliko makubwa nchini katika sekta ya huduma za ukarimu.

Programu hiyo iliyopewa jina Tugawe Feedback inalenga kuboresha jinsi sekta ya kutoa huduma za ukarimu itakavyoshughulikia wateja wao kwa kupokea maoni yao.

Ubunifu huu unaunganishwa na mifumo ya malipo ya simu kama Lipa Na Mpesa, kwa kutumia AI kuchanganua maoni ya wateja na kutoa maarifa yanayoweza kutekelezeka kupitia WhatsApp.

Mradi huo ulioundwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zetech, na umevutia washikadau wengi katika sekta ya utandawazi na teknolojia humu nchini na waundaji wake sasa wanatafuta ufadhili ili kuongeza kasi yake.

“Kitovu cha Ubunifu na Ujasiriamali cha chuo kikuu (iZet Hub) kinaendelea kuunga mkono masuluhisho yanayoongozwa na wanafunzi kukabiliana na changamoto za ulimwengu halisi. Huku uchumi wa Kenya ukikabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana waliohitimu, ubunifu kama vile Tugawe Feedback hutoa muhtasari wa jinsi teknolojia inaweza kuunda fursa,” ilisema taarifa.

 Mfumo huo pia utaboresha uzoefu wa wateja haswa katika kuendesha biashara ndogo ndogo za SMEs, hivyo kuongeza ushindani na kuimarisha uchumi.

Hii inawiana na msukumo wa serikali wa mabadiliko ya kidijitali na uwezeshaji wa vijana, kama inavyoonekana katika mipango kama vile Ajira Digital na Hustler Fund.

Lakini je, Tugawe Feedback inalenga kuboresha kwa nia gani mwingiliano kati ya wauzaji na wateja haswa katika biashara ambazo zinatumia mifumo ya kidijitali kama vile M-Pesa kufanya malipo ikizingatiwa kwamba Miamala ya kidijitali kupitia Lipa Na Mpesa ni kawaida, ilhali biashara nyingi zinatatizika kukusanya maarifa ya wateja yenye maana?

“Tugawe Feedback itaziba pengo hili kwa kutoa uchanganuzi wa kiotomatiki, wa wakati halisi, kusaidia biashara kukabiliana na mahitaji ya soko bila mbinu za gharama kubwa za uchunguzi. Ubunifu huu unazungumzia hitaji pana la kufanya maamuzi kwa kuendeshwa na data katika uchumi wa kidijitali wa Kenya,” walisema.

Kwa mujibu wa wafumbuzi wa programu hiyo ya AI, inaweza pia fanya kazi katika sekta za kurekebishwa kwa sekta nyingine zinazokabiliwa na changamoto za ushirikishaji wateja, kama vile huduma ya afya na utoaji wa huduma kwa umma.

Wanafunzi hao; Brian, Joy, na Paul wanapotafuta ufadhili ili kuongeza ubunifu wao, safari yao inaonyesha changamoto kubwa ya kufadhili biashara zinazoanza nchini Kenya.