
Magavana wametoa makataa ya siku 14 kwa serikali ya kitaifa, na kutishia kusitisha huduma katika kaunti kutokana na hatua ya kupeleka pesa za kuendesha shughuli za kaunti kwa matumizi mengine.
Wakihutubia wanahabari siku ya Ijumaa magavana hao waliitaka serikali ya kitaifa kurejesha pesa hizo, kutaka kutolewa mara moja kwa mgao wa usawazishaji wa Shilingi bilioni 78 ambao walidai ni malimbikizo ya miezi mitatu kuanzia Januari.
Magavana pia wanataka fedha za ruzuku kutoka kwa washirika wa maendeleo, zilizotengewa miradi mbali mbali katika kaunti ambazo zilielekezwa kwingine wakati wa kupitishwa kwa Mswada wa Ugavi wa Ziada wa Serikali za Kaunti, 2025 kurejeshwa.
Naibu mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Mutahi Kahiga alitaja hatua hii ya serikali ya kitaifa kama jaribio la kimakusudi la kuhujumu utoaji wa huduma katika kaunti zote 47 akisema inarudisha nyuma ajenda ya ugatuzi.
Kulingana na Kahiga, kaunti zinaweza kupoteza Sh38.4 bilioni katika mgao wa ziada, ikijumuisha Sh24 bilioni za ruzuku kutoka kwa wafadhili.
Kati ya hizo, alisema, Sh24 bilioni ni ruzuku ya kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya afya, kilimo, uvuvi, maji, barabara, uboreshaji wa makazi duni na maendeleo ya miundombinu.
Mgao mwingine wa Sh13 bilioni wa ziada kutoka kwa serikali ya kitaifa, aliongezea, ni kufadhili miradi iliyokubaliwa kwa pamoja kama vile bustani za viwanda.
Kahiga alikashifu zaidi serikali ya kitaifa, akisema kuwa kupunguzwa kwa mgao wa kaunti kunakinzana na bajeti ya serikali kuongeza kaunti Sh114 bilioni.
Wizara ya fedha imehusisha kupunguzwa kwa bajeti hiyo na viwango vya chini vya utumiaji wa mgao wa ziada katika mwaka huu wa fedha.
Hata hivyo magavana hao wamepuuzilia mbali maelezo hayo wakisema kuwa yanapotosha umma kuhusu changamoto zinazokabili serikali za kaunti.
Magavana wanadai kuwa kupunguzwa mara kwa mara kwa mgao wa kaunti ni mkakati wa kimakusudi kudhoofisha ugatuzi na kuzuia utoaji wa huduma mashinani.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!