CHINEDU Ikedieze, maarufu kama Aki katika filamu za Nollywood

CHINEDU Ikedieze. Muigizaji maarufu kwa jina la Aki kutoka Nigeria amefichua kwamba katika kipindi Fulani maishani, alikerwa na dhihaka za kuitwa mbilikimo kiasi kwamba aliwazia kujitoa uhai.

Akizungumza na mwanablogu Chude kupitia YouTube, Aki alisema kwamba maisha yake ya utotoni yalianzia kijijini na haikuwa rahisi kwani kila mtu alikuwa anamkejeli kwa kumuita mbilikimo.

Muigizaji huyo aliyepata umaarufu kupitia kwa filamu ya kitambo ya Aki na Ukwa, alisema kwamba mara ya kwanza kugundua alikuwa na tatizo la ufupi ni alipokuwa na umri wa miaka 6 wakati ndugu yake ndogo alipompita kwa urefu.

“Watu walikuwa wananikejeli kwa njia tofauti wakiniita majina mbalimbali. Nilianza kuhisi kuna kitu hakiko sawa wakati kakangu mdogo aliponipita kwa urefu nikiwa na umri wa miaka 6,” alisema.

Akiwa na umri wa miaka 9, alikuwa mgonjwa na mamake alipompeleka hospitalini, aliandikiwa ripoti ya matibabu kuhusu ufupi wake ambapo aliona majina ya Kiingereza yanayoelezea ufupi huo na kulazimika kuanza upekuzi wa kujua maana kamili ya maneno hayo.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans
×

Baadae, aligundua kwamba alikuwa na tatizo la kutokuwa mrefu na mamake aliishi kumfariji akiwambia kwamba njia pekee ya kujikomboa kimaisha ilikuwa kukumbatia masomo kwani kimo chake hakingemruhusu kufanya kazi zingine haswa za Juakali ambazo aghalabu huitaji mtu mwenye mwili mkubwa wenye nguvu.

“Mamangu kila mara angeniambia, ‘angalia, unajua wewe ni mwili mdogo na huwezi enda kubeba zege au mbao kuwa fundi seremala. Kwa hiyo njia nzuri pekee kwako ni kukumbatia vitabu. Kama unataka kutusua kimataifa, soma vitabu vyako’. Hivyo nilijua mkombozi pekee wa maisha yangu ni elimu,” Aki alisema.

Lakini shuleni hakukuwa rahisi, wanafunzi wenzake waliyafanya mazingira yake shuleni kuwa mabaya kwa kumkejeli kwamba ni mbilikimo, jambo ambalo nusra limpelekee kujitoa uhai.

“Nililia sana, nililia mara nyingi unajua walikuwa wananiita majina tofauti. Kuna wakati nilifikiria kujimaliza kabisa lakini sikuwahi waambia wazazi wangu…”

“Nilihisi kwamba dunia haikuwa na upendeleo kwangu kwa sababu hata watoto wadogo wangenikejeli bila kujali na wakati mwingine hata ndugu zangu walikuwa wanatumia majina hayo ambayo wangewapiga watoto wengine dhidi ya kuniita,” aliongeza.